Mchezo huo wa marudiano ulishuhudia Ngorongoro wakilazimishwa sare 0-0 na Kenya kama ilivyokuwa katika mchezo wa kwanza ndipo changamoto ya mikwaju ya penalti ikatumika.
Kwa ushindi huo sasa Ngorongoro watacheza na mabingwa wa dunia kwa vijana Nigeria katika raundi ya pili kati ya Mei 9-11 na mechi ya marudiano itakuwa Mei 23-25.
Wachezaji wa Ngorongoro walipata penalti zao ni Mohamed Hussein, Kelvin Friday, Mange Chagula, Idd Suleiman huku Mudathir Yahya akikosa, wakati wafungaji wa Kenya ni Hillary Dan, Timonah Wanyonyi, Victor Ndinya huku Harrison Nzivo akikosa penalti yake.
Katika mchezo huo Ngorongoro walifanya kazi kubwa ya kutafuta ushindi, lakini kikwazo chao kikubwa kilikuwa ni kipa wa Kenya, Shikhalo Faruk.
Mashuti ya washambuliaji wa Ngorongoro, Friday, Idd Selemani katika dakika 17 na 23 yalipaa juu ya lango la Kenya. Kipa Faruk alifanya kazi kubwa kupangua shuti ya Mudathir Yahya akiwa ndani ya eneo 18. Timu hizo zilikwenda mapumziko 0-0.
Ngorongoro walimtoa Hassan Banda, Ali Bilali na kuwaingiza Ibrahim Ali, Mange Chagula mabadiliko ambayo yakuweza kuwapa ushindi katika dakika 90 za mchezo huo kuamuliwa kwa penalti.