Washambuliaji hao wa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) wote wamewasili wakiwa fiti tayari kwa mchezo huo wa kwanza wa Raundi ya Pili na ya mwisho kuwania kupangwa kwenye makundi ya kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) mwakani nchini Morocco.
Mara baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam, wachezaji hao walisema kwamba wanashukuru wameruhusiwa mapema kuja kujiunga na Stars kwa ajili ya mchezo huo wa Jumapili Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
“Tunashukuru tumefika salama, tunashukuru kuruhusiwa mapema kuja kwa ajili ya mchezo huu muhimu kwa taifa letu, nasi tunawaahidi Watanzania kupigana kwa nguvu zetu zote kwa kushirikiana na wenzetu waliopo kambini Mbeya, ili kuitoa Msumbiji,”alisema Ulimwengu.
“Mimi nashukuru nimekuja nikiwa fiti, kama utakumbuka katika mchezo uliopita dhidi ya Zimbabwe nilikuwa majeruhi sikucheza, ila sasa nipo tayari kulipigania taifa langu, naomba Watanzania wajitokeze kwa wingi Jumapili kuja kutupa sapoti,”alisema Samatta kwa upande wake.
Samatta na Ulimwengu waliotua na ndege ya shirika la Misri wakitokea Tunisia ambako TP Mazembe imepiga kambi kwa ajili ya mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika, walielekea hoteli ya Courtyard katikati ya Jiji baada ya kuwasili JNIA.
Kikosi cha Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager kilichopiga kambi Tukuyu mkoani Mbeya, kinatarajiwa kurejea keshokutwa Dar es Salaam kwa maandalizi ya mwisho na Samatta na Ulimwengu wataungana na wenzao siku hiyo.
Kwa sasa wachezaji hao watakuwa wakifanya mazoezi peke yao Dar es Salaam hadi watakapoungana na wenzao Ijumaa kwa ajili ya mechi hiyo itakayochezeshwa na refa Mahmoud Ashour kutoka Misri.
Mambas nao wanatarajiwa kuwasili Dar es Salaam Ijumaa wakati mechi ya marudiano itachezwa kati ya Agosti 1 na 3 mwaka huu nchini Msumbiji.