Wakongwe wa klabu tajiri zaidi duniani Real Madrid ya Hispania ambao wako nchini Tanzania kwa ziara ya kitalii, jana walipanda mlima Kilimanjaro na kujionea baadhi ya vivutio vya mlima huo mrefu zaidi barani Afrika.
Nyota wakubwa wa soka wa zamani wa klabu hiyo wakiwamo wawili waliopata kushinda tuzo ya Ballon d'Or ya Mwanasoka Bora wa Dunia, Luis Figo na Fabio Cannavaro, walitua mkoani hapa kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), majira ya saa 5:45 asubuhi kwa ndege ya Precision na kupokewa na mwenyeji wao Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama pamoja na baadhi ya viongozi mbalimbali katika Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo.
Muda mfupi kabla ya kutua kwa ndege hiyo, tulishuhudia uwanja huo ukifurika ulinzi mkali wa jeshi la polisi, huku maafisa usalama wakipita kila kona kwa ajili ya kuimarisha usalama wa raia hao.
Baada ya hapo msafara wa wachezaji hao, ambao siku ya Jumamosi iliyopita walicheza mechi ya kirafiki dhidi ya timu ya nyota wa zamani wa soka nchini waliounda timu ya Tanzania XI na kuwafunga wenyeji wao 3-1 kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, walitua wakipokewa na mashabiki wengi.
Timu hiyo yenye nyota kama Figo, Cannavaro, Christian Karembeu na mfungaji wa mabao matatu katika mechi dhidi ya Tanzania XI, Ruben de la Red, walifika katika geti la Marangu majira ya saa 6:30 tayari kwa safari ya Kilomita 4 tu za kupanda na kujionea mandhari ya mlima huo wenye urefu wa mita 5,895. Walipanda kwa kilomita hizo chache na kuteremka.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Gama, katika risala yake iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Elinasi Pallangyo, alisema mkoa wa Kilimanjaro kwa kushirikiana na TANAPA unaamini wachezaji hao watakuwa ni mabalozi wazuri wa kuutangaza mlima huo kimataifa.
Akitoa shukrani kwa niaba ya wenzake, kiongozi wa msafara wa wakongwe hao kupanda mlima Kilimanjaro, Ramon Cobo, alisema kutokana na kile walichokishuhudia juu ya mlima huo, wanaahidi kuwa mabalozi wa Mlima huo watakapofika nyumbani kwao.
"Tumefurahi sana kupanda mlima Kilimanjaro, tumejionea vitu vingi, ni mlima wa ajabu sana, tunaamini tutakapofika nyumbani kwa umoja wetu na umaarufu tulionao kama wachezaji wa klabu maarufu duniani tutakuwa mabalozi wa mlima Kilimanjaro," alisema Cobo.
Baadaye wakongwe hao walielekea katika uwanja wa michezo wa Ushirika na kushuhudia mechi kati ya mabingwa wa Kilimanjaro, Panone FC na Machava kabla ya kuondoka kuelekea mkoani Arusha ambako jana walitarajiwa kutembelea vivutio vingine vya utalii kama vile Ngorongoro na hifadhi ya Arusha.
Akizungumza wakati wa kuwakaribisha wageni hao mkoani humo, Afisa Uhusiano wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Paschal Shelutete alisema ujio wa magwiji hao ni fursa kubwa katika juhudi za kuutangaza mlima huo na kuongeza idadi ya watalii kutoka nchi kama vile Italia, Hispania na Ureno kuja nchini kutembelea vivutio tulivyonavyo.
Rais Jakaya Kikwete akimpa tuzo ya kinyago Fabio Cannavaro Ikulu
"Leo historia imeandikwa kwa wachezaji wa zamani wa klabu ya Real Madrid ya kule Hispania kutembelea hifadhi ya mlima Kilimanjaro. Kama TANAPA tunaamini ziara hii ya kuja na kupanda mlima Kilimanjaro, itasaidia kwa kiwango kikubwa sana kuongeza idadi ya watalii kutoka kote ulimwenguni," alisema Shelutete.
Alisema, kimsingi idadi ya watalii kutoka barani Uaya ni kubwa sana kulinganisha na mabara mengine, lakini wanategemea kuona ongezeko kutoka Hispania, Ufaransa, na kwingineko duniani.
Wakati huo huo, baadhi ya wanasoka hao wakongwe wa timu ya Real Madrid, akiwamo beki wa zamani wa timu hiyo Fernando Hanz, juzi walizindua jengo la Tropical Centre linalojihusisha na uuzaji wa vifaa vya umeme lililopo Victoria, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam.
Mbali na Fernando pia alikuwapo, Mfaransa Christian Karembeu, alihudhuria katika tukio hilo lililowajumuisha magwiji wanne wa klabu hiyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Masoko wa Tropical Centre, Hubschmann Rhein, ambao ndiyo wadhamini wakubwa wa ziara hiyo alisema ujio wa wachezaji hao ni moja ya ukuaji wa utalii na biashara hapa nchini.