YANGA imemnasa kiungo, Said Juma Ally Makapu kutoka kwenye timu ya maboresho ya Taifa Stars. Makapu mwenye uwezo wa kucheza kwa ufasaha nafasi ya kiungo mkabaji, beki ya kati na kulia, amesajiliwa Yanga kwa mkataba wa miaka miwili akitokea klabu ya Shangani ya Zanzibar.
Yanga wamemwona akiichezea Taifa Stars. Ni miongoni mwa wachezaji waliochaguliwa kuchezea Taifa Stars kutoka kwenye mpango maalumu ulioandaliwa na TFF wa maboresho ya Taifa Stars.
Kikosi hicho cha Jangwani chini ya kocha mkuu, Mbrazil Marcio Maximo, kina malengo na kijana huyo mwenye miaka 18 pia watafaidika na mengi baada ya mwenyewe kujiapiza kuwa,
hawatajutia usajili wake.
Sehemu ya wadau wa soka walibeza mpango wa programu ya maboresho ya Taifa Stars lakini Yanga imejiibulia mchezaji huyo ambaye amewahakikishia watu wote kuwa atawajibu kwa vitendo.
Kabumbu limemshuhudia, Makapu katika mazoezi yake ni mchezaji anayetumia akili kwenye uchezaji, ana nguvu na yuko makini na kazi yake, hataki mzaha.
Kutokana na umri wake mdogo akilelewa katika makuzi ya namna hiyo na kupewa nafasi ya kucheza kama ilivyokuwa kwa Frank Domayo aliyesajiliwa na Azam FC kutoka Yanga atakuwa mrithi mzuri wa mchezaji huyo pamoja na Athuman Idd ‘Chuji’ aliyevunjiwa mkataba wake.
Lakini pamoja na umri wake huo, kwa mwonekano ana umbile kubwa lililojengeka kimazoezi na mrefu.“Nimesaini Yanga kwanza kazi yangu ni soka, hivyo naamini nitatoka kupitia klabu hii, pili ninaipenda tangu utotoni, nimekuwa shabiki nimejisikia furaha baada ya uongozi kunifuata.
“Na tatu ni maslahi, naamini nikiwa Yanga nitakamilisha mipango yangu yote kama nitacheza kwa malengo na kujituma kama yalivyo mawazo yangu.”
Nyota wa Yanga wakijifua ufukweni, Said Juma ni miongoni mwa wachezaji waliopo katika kikosi hicho msimu huu
Makapu ameibuliwa kwenye kikosi cha maboresho akitokea kisiwani Zanzibar na alipatikana walipokuwa wakicheza Ligi ya Mikoa yeye akichezea Mjini Magharibi.Kiungo huyo mwenye lafudhi ya Kizanzibari anapoongea anasema, hakuwa anamjua kocha yeyote na haikuwa jambo rahisi hadi akabaki Taifa Stars hadi sasa.
Kwani awali walichaguliwa wachezaji 36 ambao walipelekwa kwenye kambi hiyo Tukuyu, Mbeya. Walilelewa na kufanyiwa mchujo wakabaki 16 waliochanganywa na wakongwe wa Taifa Stars.
Baada ya hapo wale wa maboresho walipunguzwa tena na wakabaki sita na baadaye watatu ambao waliitwa hadi dakika ya mwisho yeye pamoja na kipa Benedictor Tinoco aliyesajiliwa na Kagera Sugar na beki wa kati, Joram Mgeveke aliyejiunga na Simba.
Makapu ametua kikosini hapo na kukutana na ushindani wa namba ambapo kuna wachezaji kama, Mnyarwanda Mbuyu Twite ambaye anachezeshwa kiungo mkabaji, Omega Seme na Salum Telela ambaye kwa sasa amepewa majukumu ya kucheza beki ya kulia.
Kikosi cha Taifa Stars ambacho Said Juma anakichezea
Wapo wengine ambao hucheza kiungo washambuliaji lakini wana uwezo pia wa kucheza kiungo mkabaji kulingana na mpango wa kocha kulingana na mechi husika kama, Hassan Dilunga, Hamis Thabit, Nizar Khalfan, Mnyarwanda Haruna Niyonzima ‘Fabregas’ na Mbrazili Andrey Coutinho.
“Mwanzo mgumu, lakini nitajifunza kwa waliopo na nikipata nafasi tu ya kucheza, hapo ndipo nitaonyesha uwezo wangu na kuwafanya Wanayanga kutojutia usajili wangu.”“Mpira hauna kanuni ni uwajibikaji wa mtu mwenyewe katika kujituma na kutambua wajibu wako katika kazi,kocha Maximo ni mwalimu mzuri anayewajulia wachezaji.
Kama utakwenda naye sawa na kufanya vile anavyotaka, lazima utakuwa rafiki yake,”anasema Makapu ambaye ni mzaliwa na mwenyeji wa Kisiwani Zanzibar. Amesoma Shule ya Msingi Bububu na Sekondari ya Nyuki zote za Zanzibar. Kipaji chake tangu shuleni ni kucheza mpira wa miguu.