Beki wa zamani wa Yanga, Shadrack Nsajigwa ameanza kazi rasmi ya kukinoa kikosi cha vijana cha timu hiyo (Yanga B), huku akiahidi kuwaandaa wachezaji kwa weledi.
Nsajigwa, aliyekuwa nahodha wa timu hiyo kwa misimu kadhaa, alianza kibarua chake hicho kipya jana asubuhi wakati aliposimamia mazoezi ya kikosi hicho yaliyofanyika kwenye Viwanja vya Tanganyika Packers.
Awali, kikosi cha vijana cha Yanga kilikuwa kinanolewa na kiungo wa zamani wa timu hiyo, Salvatory Edward, ambaye hivi karibuni uongozi wa klabu hiyo ulimhamishia katika benchi la ufundi la timu ya wakubwa ambako sasa ni msaidizi wa kocha Marcio Maximo.
Akizungumza mara baada ya mazoezi hayo yaliyojumuisha timu ya wakubwa ya Yanga, Nsajigwa alisema anafahamu ugumu wa kazi yake hiyo mpya, lakini atahakikisha anatumia ujuzi wake kufikia malengo.
“Nasema kwanza kabisa nazikubali changamoto nitakazokutana nazo kwa sababu ni sehemu ya kazi, lakini nitapambana ili malengo yangu yaweze kutimia,” alisema Nsajigwa.
Aliongeza: “Kazi yangu kubwa ya kwanza ni kuwaandaa wachezaji katika misingi ya kuwafanya watambue soka ni kazi kama zilivyo kazi nyingine kama unavyojua hapa kwetu Tanzania bado tunachukulia kama kitu cha ziada.
“Bahati nzuri wenzetu siku hizi wanapata kila kitu, maslahi ni mazuri na hata maandalizi wanayopata tofauti na enzi zetu sisi. Kwa hiyo kilichobaki ni kuwapa misingi ya mwanasoka anatakiwa aweje.”
Wakati huohuo; Yanga ipo mbioni kumsajili kipa wa timu ya vijana walio na umri chini ya miaka 20 ya Twalipo, Kulwa Baumba, ambaye aling’ara kwenye michuano ya Rollingstone iliyofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.
Baumba mwenye umbo zuri na mwepesi katika kuokoa hatari, amekuwa akishiriki mazoezi ya Yanga tangu michuano ya Rollingstone ilipomalizika na habari kutoka ndani ya klabu hiyo zinasema muda wowote watamalizana moja kwa moja na wamiliki wa mchezaji huyo, timu ya Twalipo.
Mazoezi yalivyokuwa:
Katika mazoezi ya jana yaliyomshuhudia beki Mbuyu Twite akirudi kundini baada ya kusumbuliwa na maumivu ya kichwa, Maximo aliendelea kutilia mkazo upigaji wa mashuti na matumizi ya krosi kufunga mabao.
Pia, Maximo ambaye alirejesha mwako wa kuipenda timu ya taifa wakati alipokuja nchini kwa mara ya kwanza, aliendelea kuimarisha pumzi za wachezaji wake kwa mazoezi ya kukimbia na ‘push ups’, ambazo amekuwa akizitunia kama utaratibu wake wa kawaida wa kukamilisha mazoezi ya siku.