come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

STARS KUTUA MSUMBIJI JIONI YA LEO

Msafara wa kikosi cha Taifa Stars utaondoka Afrika Kusini leo kwenda Maputo, kwa ajili ya pambano la marudiano dhidi ya Msumbiji  ‘Mambas’ litakalochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Nampeto.

Katika pambano la kwanza lililopigwa wiki mbili zilizopita kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Stars ililazimishwa sare ya mabao 2-2, hivyo inahitaji ushindi kwenye mchezo wa Jumapili ili kusonga mbele.

Kabla ya safari ya Maputo leo, kikosi cha Taifa Stars, ambacho kipo jijini Johannesburg tangu juzi, kitafanya mazoezi mepesi asubuhi hii kwenye Uwanja wa Bedfordview Country Club.


Pia, kikosi cha Stars ambacho kinanolewa na Mdachi Martinus Nooij, kilifanya mazoezi kwenye uwanja huo jana asubuhi na jioni.

Akizungumza kwa simu kutoka Afrika Kusini, ofisa habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura (pichani) alisema: “Kwa ujumla wachezaji wote wapo katika hali nzuri kiakili na kimwili wakiwa na morali wa hali ya juu wa kutaka kushinda mchezo wa Jumapili.”

Wakati huohuo, balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Razia Msuya jana alitarajiwa kuitembelea kambi ya Taifa Stars pamoja na ile timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 17, Serengeti Boys.

Serengeti Boys imeweka kambi jijini Johannesburg tangu Julai 27 ikisubiri kuumana na Afrika Kusini kesho katika pambano la kusaka tiketi ya kushiriki fainali za Mataifa ya Afrika.