Wakati Simba ikibainika kumsajili kinyemela Saad Kipanga, Mbeya City imedai suala la mshambuliaji huyo litawafanya “kufikishana pabaya”.
Kipanga bado ana mkataba wa mwaka mmoja na Mbeya City, lakini Simba inadaiwa tayari imemalizana naye kwa kumpa mkataba wa miaka miwili.
Kwa mujibu wa kanuni za usajili, klabu inaweza kumnunua mchezaji bila ya kuwasiliana na klabu inayommiliki katika kipindi cha ndani ya miezi sita kabla ya mkataba wake kumalizika.
Awali, Simba walimfuatilia mchezaji huyo lakini baadaye wakaamua kuachana naye baada ya kubaini amebakiza mwaka mmoja kwenye mkataba wake na hivyo kugeukia kwa mshambuliaji wa Ruvu Shooting, Elius Maguri.
Hata hivyo, inadaiwa kuna kiongozi mmoja aliamua kumsajili Kipanga, jambo ambalo viongozi wengi wa Simba hawakuliafiki na kuzua mvutano mkubwa kwani tayari awali walishaamua kuwa mchezaji huyo asisajiliwe.
Katibu mkuu wa Mbeya City, Emmanuel Kimbe aliliambia gazeti hili jana kuwa wanachojua kwa sasa mchezaji huyo ni wao kwani bado ana mkataba na kama Simba wamemsajili ‘imekula kwao.’
“Hayo mengine tunasikia tu. Kama Simba wamefanya hivyo ni uvunjifu wa kanuni za usajili, hivyo tutabanana husika,” alisema.