KIUNGO wa mabingwa wa soka Afrika Mashariki na Kati, Haruna
Niyonzima 'Fabregas' amewashangaa Yanga kwa kukubali visingizio vya
Simba kwamba inatumia wachezaji yosso na amewaambia kuwa wasikubali
kuzugwa.
Haruna ametamka kwamba wao wachezaji wa Yanga
walioko kambini Zanzibar wanajua wanakumbana na Simba kamili kwavile
wanawajua vilivyo kiumri wachezaji wa Simba 'wanaolazimishwa' kuitwa
yosso.
Kiraka huyo anasema kwamba tofauti ya kikosi cha
Yanga na kile cha Simba ni maumbo ya wachezaji na uzoefu tu wala si
kweli kwamba ni wadogo na hata kama ni wadogo ndio walioaminika kwa
kocha kuliko wakongwe waliosimamishwa.
Alisema mara nyingi mtoto si mchezaji na kama wao
(Simba) wana wachezaji watoto, basi wangebaki nyumbani na wazazi wao na
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lisingewaruhusu kucheza soka.
“Simba inaundwa na wachezaji wengi wenye uzoefu na
wachache wanaodaiwa kuwa ni watoto ambao wamekosa uzoefu, wasitafute
sababu, wameweza kushinda, kutoka sare na timu hiyo na kufungwa wakiwa
na timu hiyo, huko kote wasiseme watoto, wakikaribia na Yanga wanadai
kuwa ni watoto, hiyo si kutafuta sababu?” alisema Niyonzima.
Wachezaji wa Simba ambao wana uzoefu ni Juma
Kaseja, Abel Dhaira, Nassoro “Chollo” Masoud, Mussa Mude, Mrisho Ngassa,
Amri Kiemba, Felix Sunzu, Mwinyi Kazimoto, Haruna Chanongo na Shomari
Kapombe.
Kwa mujibu wa Niyonzima, Yanga ina wachezaji wengi
ambao umri wao hautofautiani na wanaodaiwa kuwa ni yosso wa Simba
watakaocheza nao Jumamosi jijini Dar es Salaam.
“Tuna kina Frank Domayo, David Luhende, Simon
Msuva na wengine wengi, mbona sisi hatusemi ni watoto, waache kutafuta
sababu,” alisema na kuwasisitiza mashabiki kuja uwanjani wakiwa
wamejiamini na kuwashangilia kwa nguvu wawape raha na mvua ya mabao.
Haruna alisema wamejiandaa kupambana haswa kuibuka
na ushindi na si lazima wapate mabao matano ila wanayataka. “Ushindi ni
lazima, iwe mabao matano, zaidi ya matano, pungufu ya hayo, sisi kwetu
ni muhimu kuwapa raha mashabiki na wala si vinginevyo."
Alifafanua kuwa wao hawadharau kikosi cha Simba na
wanakichukulia kuwa ndicho sahihi; "Hao wachezaji wamewaondoa wao
katika kikosi kwa maana hiyo wamekiamini kikosi chao, wasubiri matokeo
yake kujua mwelekeo wao, sisi tupo tayari kwa mapambano."
Alisema kuwa hakutakuwa na maana ya Yanga kuwa
bingwa halafu wanafungwa na Simba katika mchezo ambao wanaamini kombe
litakuwa uwanjani tayari kwa makabidhiano.
“Tuna kikosi kizuri, nawaomba wachezaji wenzangu
wasibweteke na ubingwa tulionao, kuifunga Simba ni kitu muhimu sana
kuliko kitu chochote, mashabiki na wanachama wanataka kuona sisi
tunawapa raha, hakuna mchezo siku hiyo,” alisema.