SHIRIKISHO la Ngumi za Ridhaa Tanzania (BFT), limesema hatima ya uchaguzi wake mkuu itajulikana baadaye.
Awali uchaguzi huo ulipangwa kufanyika Julai 7 jijini Mwanza, lakini ilishindikana kutokana na uchache wa wagombea waliojitokeza kuchukua fomu za kuwania uongozi na wajumbe wa mkutano huo kugomea.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa BFT, Makore Mashaga (Pichani), alisema uchaguzi huo utafanyika mwaka huu lakini tarehe mpya itatangazwa hivi karibuni.
“Kwa sasa tunashughulikia mipango ya uchaguzi na ikikamilika ndipo tutakapotangaza rasmi kufanyika kwa uchaguzi huu wa viongozi,” alisema Mashaga na kuongeza kuwa kumekuwa na migogoro kwa baadhi ya vyama vya michezo, hasa linapoingia suala la uchaguzi, ambapo hujitokeza malalamiko na mwingiliano wa hapa na pale hatimaye uchaguzi kuahirishwa mara kwa mara.
