come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

HAMIS KIIZA AMALIZANA NA YANGA

Mshambuliaji wa kimataifa, Hamisi Kiiza
Hatimaye mshambuliaji wa kimataifa kuwa Uganda, Hamisi Kiiza, amekubali kusaini mkataba mpya wa kuendelea kuichezea klabu yake ya Yanga inayoshikilia ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwa dau la dola za Marekani 40,000 (Sh. milioni 64).

Hata hivyo, Kiiza ambaye pia huichezea timu ya soka ya taifa ya Uganda (Uganda Cranes) amekubali kumwaga wino wa kuichezea Yanga baada ya kuahidiwa kulipwa kiasi hicho cha fedha kwa awamu mbili.

Akizungumza jana, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Mussa Katabaro, alisema kuwa wamefikia hatua nzuri ya mazungumzo na mshambuliaji huyo kwa ajili ya kurejea nchini kuitumikia timu hiyo katika msimu ujao.

Katabaro alisema kuwa hivi sasa, kilichobakia ni kukamilisha mazungumzo ya kiasi cha mshahara ambacho mshambuliaji hiyo anayetakiwa na URA ya Uganda atapatiwa.

"Ni kweli tumekubaliana mambo fulani ya msingi na tutakapokamilisha kwa asilimia mia moja ndipo atakapotua nchini na kuweka mambo yote hadharani kama tulivyofanya kwa wachezaji wetu wengine," alisema Katabaro.

Aliongeza kuwa Kiiza atarejea nchini mwishoni mwa wiki kusaini rasmi mkataba mpya na kujiunga na kikosi cha timu hiyo ambacho kimeanza maandalizi ya msimu ujao.

Kabla Kiiza hajaondoka nchini kurejea kwao baada ya kumalizika kwa msimu, aliieleza Yanga kwamba atakuwa tayari kusaini mkataba mpya kwa dau la dola za Marekani 45,000 (Sh. milioni 72) na mashahara wa kila mwezi wa dola za Marekani 3,500 (Sh. milioni 5.4).

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Abdallah Binkleb, aliuambia mtandao huu kwamba Yanga haina uwezo wa kulipa kiasi hicho cha mshahara na inafanya maamuzi kulingana na hali ya kifedha ya klabu yao.

Binkleb alisema vilevile kuwa mbali na fedha hizo, pia mchezaji huyo alisema anahitaji kupatiwa nyumba ya kuishi na gari la kutembelea ambavyo tayari klabu imeshajiandaa kumpatia.

Kiiza ni miongoni mwa wachezaji nyota walioisaidia Yanga kutwaa 'kiulaini' ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya kuwaacha Azam waliokuwa wakiwafuatia katika nafasi ya pili kwa tofauti ya pointi 10.