come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

STARS WAJIFUA MCHANA KWEUPE KUWAKABILI UGANDA

Beki wa timu ya Taifa Stars ,Erasto Nyoni akiruka juu kumiliki mpira huku akishuhudiwa na wachezaji wenzake Juma Luizo(wa pili kulia)na Haruna Chanongo(kulia)wakati wa mazoezi yao ya kujiandaa kuikabili Uganda katika mechi ya kuwania kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani(CHAN)
 
Kikosi cha timu ya soka ya Tanzania (Taifa Stars) kimeanza utaratibu wa kufanya mazoezi kuanzia saa 9:00 alasiri kwa nia ya kujiimarisha kabla ya kuwakabili Uganda (Uganda Cranes) katika mechi yao ya kwanza ya kuwania kufuzu kwa fainali zijazo za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani (CHAN) itakayochezwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Akizungumza jana, Meneja wa Taifa Stars, Leopord Tasso Mukebezi, alisema kuwa wanajifua mchana kwa sababu ndiyo muda ambao mechi hiyo itachezwa Jumamosi na kwamba hadi sasa, maandalizi yao yanaendelea vyema..
"Timu iko vizuri na vijana wote ni wazima, hakuna majeruhi kikosini na tunaendelea na programu zetu kama tulivyopanga," alisema meneja huyo.

Uganda ambao wananolewa na kocha wa zamani wa Yanga, Mserbia Sredojovic Milutin 'Micho', wanatarajiwa kutua nchini keshokutwa kujiandaa na mechi hiyo inayotarajiwa kuwa na ushindani mkali kutokana na ukweli kuwa timu hizo hukutana mara kwa mara katika mashindano ya Kombe la Chalenji.

Mwaka 2007 katika mashindano hayo Uganda Cranes ilitolewa na Taifa Stars iliyokuwa chini ya Mbrazil Marcio Maximo kwa kipigo cha jumla ya magoli 3-2 na mwishowe Stars ikafuzu kwa fainali za kwanza za CHAN zilizofanyika nchini Ivory Coast.

Fainali zijazo za CHAN zitafanyika mwakani nchini Afrika Kusini.