Hivi karibuni uongozi wa Simba ulitangaza kuachana
na Kaseja kwa kile walichodai kuwa ameporomoka kiwango chake licha ya
kuwa bado ni kipa namba moja wa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’.
Akizungumza jana, Mexime alisema kuwa
timu yake ipo tayari kumpokea kipa huyo ambaye aliitumikia Simba kwa
zaidi ya miaka tisa kwa mafanikio makubwa.
Alisema hivi sasa wapo mkao wa kula kwa ajili ya
kumnasa kipa huyo, lakini zoezi hilo litachukua kasi zaidi endapo kipa
namba moja wa Mtibwa, Mohamed Sharifu atafanikiwa kujiunga na kikosi cha
FC Lupopo ya Jamhuri ya Kidemokorasia ya Congo ambayo inamtaka.
“Kaseja ni kipa mzuri, bado ana uwezo mkubwa wa
kulinda lango ukilinganisha na makipa wengine wengi hapa nchini licha
watu wengi kudai kuwa kiwango chake kimeporomoka.
“Kwa upande wangu milango ipo wazi na nipo tayari
kumpokea, tunaweza kumsajili kama kipa wetu Mohamed Sharifu la atajiunga
na FC Lupopo,” alisema Mexime.
Sharifu anatarajia kujiunga na FC Lupopo baada ya
kufanikiwa kufanya vizuri katika majaribio yake na klabu hiyo kongwe ya
nchini DRC.
Hivi sasa uongozi wa Mtibwa Sugar na ule wa FC
Lupopo upo kwenye mazungumzo kwa ajili ya kukamilisha dili hilo, ambalo
pia linaweza kumpatia ulaji Kaseja ambaye sasa yupo na kikosi cha Taifa
Stars kinachojiandaa na mchezo dhidi ya Uganda wa kuwania kufuzu
kushiriki fainali za Afrika kwa wachezaji wa ndani CHAN.