YANGA imeweka wazi jeshi lake la wanaume 25 watakaotetea heshima
ya timu hiyo msimu ujao kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na Ligi Kuu Bara
huku Kamati ya Usajili ikisisitiza kuwa inakamilisha usajili wa straika
mmoja matata wa kigeni.
Katika orodha hiyo Yanga imewapiga chini wachezaji
wazoefu waliokuwa kwenye safu ya ulinzi wakiongozwa na nahodha Shadrack
Nsajigwa huku wengine wenye mkataba wakitolewa kwa mkopo kwenye timu
zilizopanda daraja msimu huu.
Habari za uhakika ambazo mtandao huu imezipata
kutoka ndani ya Kamati ya Usajili zimebainisha kuwa wachezaji ambao
kamati imeafikiana watemwe ni Shadrack Nsajigwa (ambaye atapewa majukumu
kwenye benchi la ufundi), Nurdin Bakari, Yaw Berko, Godfrey Taita,
Shamte Ali, Rashid Gumbo, Stephano Mwasyika, Idrisa Rashid na kipa Said
Mohamed ingawa Hamis Kiiza bado suala lake limewekwa pembeni kwa muda.
“Tunafanya makubaliano na straika mmoja wa kigeni
lakini ikishindikana tutabaki na Kiiza,”alisema kigogo mmoja wa kamati
hiyo na kutaja watakaotolewa kwa mkopo kuwa ni Ibrahim Job (anatafutiwa
timu), Ladislaus Mbogo (Rhino ya Tabora), Omega Seme (Tanzania
Prisons), Rehani Kibingu na John Banda (Ashanti United).
Kwa mujibu wa kiongozi huyo ni kwamba kikosi kipya
kitakuwa na wachezaji 25 tu wanne kati yao wakiwa wa kigeni. Makipa:
Ali Mustafa, Deo Munishi na Yusuph Abdul.
Mabeki wa kulia ni Mbuyu Twite na Juma Abdul huku
kushoto wakisimama David Luhende na Oscar Joshua na mabeki wa kati ni
Nadir Haroub, Kelvin Yondani na Rajab Zahir.
Viungo ni Athuman Idd, Frank Domayo, Haruna
Niyonzima, Simon Msuva, Salum Telela, Reliants Lusajo, Nizar Khalfan na
mastraika ni Didier Kavumbagu, Jerryson Tegete, Mrisho Ngassa, Shaaban
Kondo na Hussein Javu.
Orodha ya sasa ambayo Kabumbu Spoti imeishuhudia
inaonyesha kikosi kina wachezaji 22 lakini kiongozi huyo amesisitiza
kwamba watatu waliosalia mmoja ni straika huyo wa kigeni ambaye amedai
kwamba atatoka kwenye nchi moja ya Afrika ya Magharibi na wengine wawili
watachaguliwa kwenye timu ya vijana ya Yanga.
Mwanaspoti ilimtafuta bosi wa usajili wa Yanga
ambaye licha ya kutotaka kuweka bayana majina alisisitiza kwa kifupi
kwamba; “Kwa sasa hatusajili tena wachezaji wa ndani, macho yetu yapo
kwa mchezaji mmoja kutoka nje ya nchi ambaye tutamtangaza muda si mrefu.
Tumefikisha asilimia 99 ya usajili tunasubiri hatma ya straika mmoja tu
ambaye anatoka nje ya nchi,” alisema Abdalla Bin Kleb.
Bin Kleb alikiri kwamba uwezekano wa Kiiza na
Kabange Twite kuendelea kuwemo Yanga itategemea na huruma na mipango ya
Kocha Ernest Brandts ambaye anawasili leo Jumanne kutoka Uholanzi
alikokuwa likizo.