MWANAMICHEZO mkongwe nchini, Kadatta K. Kadatta, aliyepata ajali ya pikipiki na kuvunjika mguu wa kulia, ameomba msaada wa hali na mali kwa wenye mapenzi mema na wengine ili aweze kukabiliana na gharama za matibabu kiasi cha sh 1,260,000.
Kadatta aliyepata ajali hiyo Juni 29 katika eneo la Magomeni na kulazwa Wodi ya Sewa Haji, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, jijini Dar es Salaam na kufanyiwa upasuaji siku iliyofuata, alisema aligongwa siku hiyo majira ya saa 2 usiku.
Akizungumza jana, Kadatta akiwa kwenye mazingira ya kutembea kwa msaada wa magongo mawili, alisema anahitaji msaada huo ili aweze kukabiliana na gharama kubwa ya matibabu yanayotakiwa ili kupona kikamilifu.
“Nawaomba wadau wa michezo kokote walipo nchini wakiwemo viongozi mbalimbali wanisaidie kwa hali na mali niweze kumudu gharama za matibabu ambazo zinatakiwa ili mguu wangu uweze kupona vizuri,” alisema Kadatta.
Kadatta aliyewahi kujitosa mara kadhaa bila mafanikio katika chaguzi za ngazi ya taifa (wakati huo FAT), alisema kwa mwenye kuguswa na tatizo lake anaweza kumfikishia msaada wake kupitia namba 0653-777899 au 0787-777199.
Kadatta aliyebobea katika masuala ya utawala wa soka, mara kadhaa amekuwa akileta timu za nje kucheza mechi za kirafiki kwa lengo la kupandisha kiwango cha soka nchini.