MPIGA tumba wa bendi ya Extra Bongo ‘Wazee wa Kizigo’ Salum Chakuku ‘Chakuku Tumba’ (Kushoto) amenusurika kufa baada ya kuvamiwa na vibaka waliomkata sikio la kushoto huku wakiliacha likining’inia.
Tukio hilo lilitokea mwishoni mwa wiki iliyopita, baada ya kundi la vibaka hao kumvamia eneo la Mbagala Mzinga wakati akitokea kwenye onesho la bendi hiyo lililofanyika ukumbi wa Meeda, Sinza jijini Dar es Salaam.
Akizungumza jana, Chakuku alisema, baada ya sakata hilo, alikimbizwa Hospitali ya Mbagala kupatiwa matibabu na sasa anaendelea vizuri, japokuwa anasikia maumivu makali na kudai kuwa alijitahidi kupambana na kundi hilo, lakini alizidiwa nguvu na kukatwa sikio lake.
“Kundi lilikuwa na watu wengi wakiwa na mapanga, visu na vifaa vingine, ila mmoja wao alinipiga na panga kwenye sikio nikashangaa kuona damu na nilipoangalia nikaona sikio limening’inia na nikashonwa nyuzi tano, maana sikio lilikuwa linakaribia kukatika lote,” alisema Chakuku.
Aliongeza kuwa, aliripoti Kituo cha Polisi Kongowe na kufunguliwa jalada lenye kumbukumbu KON/RB/1038/2013 na kudai kumtambua kibaka mmoja kuwa ni Faraji Shaibu, maarufu kama ‘Dazi’, ingawa bado hajakamatwa.