Aidha, timu yake ya Yanga, ambayo ndiyo bingwa wa msimu huo, ilitawazwa kuwa timu yenye nidhamu.
Yanga, ambao waliwakilishwa na Katibu Mkuu, Lawrence Mwalusako na Afisa Habari, Baraka Kizuguto, walilamba jumla ya Sh. milioni 90, ikiwa zawadi ya ubingwa (Sh. milioni 70), timu yenye nidhamu (Sh. milioni 15) na mchezaji bora (Sh.milioni 5).
Tuzo ya kocha bora ilienda kwa Abdallah Kibadeni 'King' aliyeiwezesha Kagera Sugar kushika nafasi ya nne na kuzima mitazamo kwamba tuzo hiyo ingebebwa na kocha wa Yanga, Mholanzi Ernie Brandts aliyeikuta timu katika hali mbaya mkiani baada ya kumfukuza kocha Mbelgiji Tom Saintfiet na kuiongoza bila ya kupoteza mechi katika utawala wake hadi kutwaa ubingwa.
Refa wa kati Simon Mberwa wa Pwani alitwaa tuzo ya mwamuzi bora. Mberwa na Kibadeni walipatiwa Sh. milioni 7.5 kila mmoja.
Mshambuliaji Kipre Tchetche wa Azam aliyefunga magoli 17 katika mechi 24 alizocheza, alikabidhiwa Sh. milioni 5 baada ya raia huyo wa Ivory Coast, ambao ni vinara wa ubora wa soka barani, kuibuka mfungaji bora ligi hiyo.
Msimu wa 2011/12 tuzo hiyo hiyo ilinyakuliwa na mshambuliaji John Bocco 'Adebayor' wa Azam pia aliyefunga magoli 19 huku tuzo ya mwamuzi bora ikitua kwa refa wa kati Martin Saanya wa Morogoro.
Tofauti na ilivyotarajiwa na wengi kwamba Ally Mustafa 'Barthez' wa Yanga angetwaa tuzo ya kipa bora kwa kufungwa magoli machache zaidi na kuisaidia timu yake kuwa bingwa, zawadi hiyo ya Sh. milioni 5 ilikwenda jijini Mbeya kwa kipa David Bulhan wa klabu ya 'maafande' wa Tanzania Prisons ambao walilazimika kushinda mechi za mwishoni kukwepa kushuka daraja.
Akizungumza kabla ya kuanza kutunuku tuzo, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka (TFF), Angetile Osiah ambaye alikuwa amemwakilisha rais wa shirikisho hilo, Leodegar Tenga, alisema wamezingatia takwimu za wahusika katika kutoa tuzo hizo.
"Tuzo hizi zina tofauti kubwa na tuzo zilizotolewa na Sputanza (Chama cha Wachezaji) wiki iliyopita. Wao walipiga kura lakini Kamati ya Ligi imezingatia takwimu za wachezaji wetu msimu uliopita," alisema Osiah.
Wadhamini wa ligi hiyo, kampuni ya huduma za simu ya Vodacom Tanzania pia walikabidhi hundi za Sh. milioni 35, Sh. milioni 25 na Sh. milioni 20 kwa timu zilizoshika nafasi ya pili, tatu na nne ambazo ni Azam, Simba na Kagera Sugar.
Mbali na zawadi hizo, TFF kupitia kamati yake ya ligi, ilitoa zawadi ya Sh. milioni 5 kwa mchezaji mwenye nidhamu, tuzo ambayo ilichukuliwa na Fully Maganda wa Mgambo JKT.
Shirikisho hilo pia lilitoa zawadi ya Sh. milioni 6 kwa wachezaji chipukizi sita waliotumika zaidi (waliocheza mechi nyingi) msimu uliopita. Yosso hao ambao kila mmoja aliweka kibindoni Sh. milioni moja ni Abdulrahim Mussa na Hassan Dilunga (Ruvu Shootings), Chande Magoja na Ton Kavishe (Mgambo JKT), Hamis Saleh (JKT Oljoro) na Rajab Zahir wa Mtibwa Sugar.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ligi ya TFF, Wallace Karia alisema wameamua kutoa zawadi kwa mchezaji mwenye nidhamu na yosso kwa sababu zawadi hizo hazikuwamo kwenye orodha (vipengele) ya wadhamini (Vodacom Tanzania).
Msimu wa 2011/12 kamati hiyo ilitoa zawadi kwa yosso watatu tu.
"Nawapongeza TFF na Vodacom kwa kusaidia kukuza mpira wa miguu ambao kwa sasa una hamasa kubwa nchini na unatengeneza ajira kwa vijana," alisema Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara wakati wa hotuba yake fupi katika hafla hiyo ambayo alikuwa mgeni rasmi.
"Ligi yetu imekuwa na ushindani mkali hali ambayo pia imesaidia kuimarika kwa timu yetu ya taifa. Taifa Stars inaogopwa, hata na mataifa makubwa kisoka. Mechi yetu tuliyocheza dhidi ya Ivory Coast ni kipimo tosha cha timu yetu. Licha ya kupoteza 4-2, timu yetu ilicheza vizuri," aliongeza waziri huyo aliyekuwa amefuatana na Mkurugenzi Msaidizi wa Maendeleo ya Michezo, Juliana Yassoda.
Ikumbukwe kuwa Yanga awali walikuwa wamekataa kushiriki hafla ya kukabidhi zawadi hizo kwa madai kwamba zawadi hizo zilikuwa zimecheleweshwa. Hata hivyo, walihudhuria baada ya Makamu Mwenyekiti, Clement Sanga, ambaye alikuwa nje wakati sakata hilo linafukuta, kuwashauri viongozi wenzake waende kupokea zawadi zao za ubingwa.
Hiyo haikuwa mara ya kwanza Vodacom na Yanga kupishana "Kiswahili" kwani mwanzoni mwa msimu uliopita 'Wanajangwani' walizua 'timbwiri' jingine la kugoma kuvaa jezi zenye nembo nyekundu ya wadhamini hadi walipopewa jezi zenye nembo nyeusi.