WAKATI ikiripotiwa mshambuliaji wa kimataifa wa Yanga aliyemaliza mkataba wake, Mganda Hamis Kiiza, kuitosa timu hiyo, ameibuka na kudai bado hajapata timu ya kuichezea msimu ujao, japokuwa wakala wake anaendelea na mazungumzo na uongozi wa klabu hiyo.
Kiiza alimaliza mkataba wake mara baada ya kumalizika kwa Ligi Kuu ya Vodacom Mei 18 na kushindwa kuongeza mkataba baada ya uongozi wa Yanga kushindwa kuafikia dau alilokuwa akilitaka, kabla ya kuripotiwa kutua URA ya Uganda.
Akizungumza na Tanzania Daima kwa simu akiwa nchini Uganda jana, Kiiza alisema anashangaa kusikia uvumi kuwa amesaini mkataba na URA, kwani hadi sasa hana timu na ni mchezaji huru.
“Mimi ndiyo kwanza nakusikia wewe unasema, sijasaini timu yoyote mpaka sasa, hata hiyo URA, ndo kwanza nasikia wewe unasema na mimi sijui chochote, labda wakala wangu awe amesaini mwenyewe,” alisema Kiiza.
Aidha, Kiiza aliongeza kuwa hata katika mechi inayosemwa URA kucheza na Simba Julai 20, kama kweli amemwaga wino ataonekana na kikosi cha timu hiyo na kuwataka Wanajangwani kutulia, kwani bado wakala wake anaendelea na mazungumzo na viongozi wa Yanga.
“Wakala wangu ndiye anafanya kazi nzima ya mimi wapi niende na kila kitu ananiambia, huo ni uvumi tu ambao hata mimi sielewi kabisa, siku ya hiyo mechi watoe macho labda wanaweza kuniona,” alisema Kiiza.
Juhudi za kuwapata viongozi wa Yanga kuzungumzia hilo ziligonga mwamba kutokana na simu zao kuita bila kupokelewa