
Kocha wa Taifa Stars, Kim Poulsen
Akizungumza baada ya mechi hiyo ya kuwania tiketi ya kushiriki fainali za Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani (CHAN) ambayo Stars ililala kwa goli 1-0, Poulsen alisema kuwa mfungo kwa baadhi ya nyota wake ulichangia kupoteza mchezo huo kwa kuwa wachezaji wake wengi hawakuwa na nguvu kwenye mchezo huo.
Wachezaji wanne Waislamu walioanza katika mechi hiyo walikuwa ni kipa Juma Kaseja, viungo Amri Kiemba na Mwinyi Kazimoto pamoja na mshambuliaji Mrisho Ngassa. Mshambuliaji wa Simba, Haruna Chanongo aliingia baadaye.
"Huwezi kuwa katika nguvu na ile ile ikiwa kuanzia asubuhi hadi muda wa mchezo unapokuwa hujala kitu, sitaki kuwalaumu wachezaji kwa kupoteza mchezo dhidi ya Uganda...., lakini kama kocha naona mfungo umechangia kwa kiasi kikubwa kucheza chini ya kiwango na kupoteza mchezo huu... lakini jambo hili ni la kawaida kwa sababu wachezaji nao wana imani zao na tunapaswa kuheshimu hilo," alisema Poulsen.
Alisema kuwa wachezaji wote walijitahidi kucheza vizuri lakini bahati haikuwa kwao.
"Timu ilijitahidi kucheza vizuri lakini siku zote kama hamfungi goli ni ngumu kusema tumecheza vizuri... tulitengeneza nafasi nyingi za kufunga lakini hatukuzitumia, wenzetu walipata nafasi moja wakaitumia ndiyo mpira ulivyo," aliongeza.
Hata hivyo, Poulsen alisema bado hajakata tamaa ya kufuzu kushiriki fainali hizo.
"Katika soka ni lazima mjiamini. Tumeshuhudia timu mbalimbali zikifanya vizuri baada ya kuanza kufungwa katika mechi zao za kwanza, ninaamini Kampala tutafanya vizuri na kushinda," aliongeza kocha huyo raia wa Denmark.
Alisema kwa sasa wanajipanga kuhakikisha wanatumia vyema nafasi watakazozitengeneza kwenye mechi ya marudiano nchini Uganda kwani ni ushindi pekee utakaowafanya kufuzu kucheza fainali za CHAN zitakazofanyika Januari mwakani nchini Afrika Kusini.
Mechi ya marudiano itachezwa kati ya Julai 26 na 28 mwaka huu kwenye Uwanja wa Nelson Mandela ulioko Namboole nje kidogo ya Jiji la Kampala. Tarehe rasmi itapangwa na Shirikisho la Vyama vya Mpira wa Miguu vya Uganda (FUFA) siku kumi kabla ya mechi.
Ili kufuzu, Stars itahitaji kushinda kwa tofauti ya magoli mawili katika ardhi ya Uganda, ambapo wenyeji hawajafungwa kwa miaka nane tangu 2005 wakati penati ya utata ilipowapa Bafana Bafana ya Afrika Kusini ushindi 1-0 kwenye Uwanja wa Mandela.
Kocha mkuu wa Uganda Cranes, Sredojovic Milutin 'Micho' aliwapongeza wachezaji wake kwa ushindi walioupata na kusema kuwa kazi bado haijaisha.
Micho alisema kwamba hiyo ni mechi ya kwanza na wanatakiwa kuongeza bidii ili washinde katika mchezo wa marudiano kwa sababu goli moja haliwafanyi wabweteke.
"Tutaendelea kujiandaa, ushindi huu hautatufanya tubweteke, tutaongeza juhudi," alisema kocha huyo wa zamani wa Yanga ambaye pia alikuwa akisaidiwa na Sam Timbe, aliyewahi pia kuwafundisha mabingwa hao wa Ligi Kuu ya Bara.