
Rais wa TFF, Leodegar Tenga.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Tenga aliyechaguliwa kwa mara ya kwanza kuwa Rais wa TFF mwaka 2004 alisema kuwa miaka tisa ya uongozi aliyokaa madarakani inamtosha na ameamua kutogombea tena uongozi ili wadau wengine wajitokeze kuwania nafasi hiyo na kujenga utaratibu wa kuachiana madaraka.
Tenga alisema kuwa anawashukuru wajumbe wa mkutano mkuu wa kupitisha marekebisho ya katiba kama walivyotarajia ili mchakato wa kupata viongozi wapya wa soka nchini upatikane na amewataka wagombea kuhakikisha wanashiriki kwenye zoezi hilo kistaarabu.
"Siwezi kugombea, sifikirii hata kidogo, sijui huko mbele lakini kwa sasa hapana, naomba msajili atupitishie katiba yetu mpya ya mwaka 2013 ili tuanze mchakato wa uchaguzi wenye hadhi ya mpira, kiistaarabu, wagombea watoe sera zao, kuzungumza ovyo haikubaliki," alisema Tenga.
Alieleza kuwa TFF ni moja ya vyama na taasisi zinazofuatiliwa sana hivyo ni lazima viongozi watakaochaguliwa wawe na heshima na maadili yanayoendana na hadhi ya mchezo husika.
"Tutasaidia ili wapatikane viongozi na tumefanya hivi ili haki itendeke na ionekane imetendeka, tunataka uchaguzi huru na wa haki," aliongeza Tenga.
Alisema pia anataka waelekee katika uchaguzi bila ya kuwa na makundi lakini akikubaliana wadau kutofautiana mawazo.
Alisema pia baada ya mabadiliko hayo ya katiba kufanyika, sasa kutakuwa na Kamati ya Maadili na Kamati ya Rufaa ya Maadili.
Vile vile alieleza kuwa adhabu za makosa 11 yatakayojitokeza zimewekwa wazi ambapo sasa faini yake itakuwa ni kati ya Sh. milioni 10 pamoja na kifungo.
Rais huyo alisema kuwa leo shirikisho hilo linatarajia kupeleka rasimu ya katiba yake katika ofisi ya Msajili wa Vyama na Klabu za Michezo Nchini kwa ajili ya kuisajili ili mchakato wa uchaguzi mkuu wa shirikisho hilo uanze mapema kama ilivyotarajiwa.
Alisema kuwa baada ya marekebisho hayo sasa kanuni za ndani na nje ya uwanja zimepatikana