MANCHESTER City imeanzisha vita mpya na majirani zao Manchester
United baada ya kutangaza wameingia kwenye mbio za kumnasa mpachika
mabao wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo.
Manchester City ipo tayari kutumia kiasi kikubwa cha fedha kumsajili staa huyo wa zamani wa Manchester United.
Mmiliki wa klabu sasa hataki mchezo na yupo tayari
kutoa dau kubwa iwezekanavyo na ameahidi kutoa mshahara wa pauni
300,000 kwa nyota huyo iwapo atakubali kutua Etihad.
Kwa miezi mitano, Manchester United imekuwa
ikijaribu kumshawishi mchezaji huyo mwenye miaka 28 bila ya mafanikio na
hawajakata tamaa, wanaendelea kumshawishi.
Man City wanafahamu kuwa vita hiyo ni kali lakini
wanaamini fedha ndiyo fimbo muhimu. Viongozi wa Manchester City
wanaishawishi Real Madrid imweke sokoni mchezaji huyo na kama wakikubali
jambo hilo, watatoa kiasi kikubwa cha fedha.
Mmiliki wa Man City, Sheikh Mansour amewaambia
viongozi wa juu wa klabu kuwa wanatakiwa kufanya kila liwezekanalo
kumnasa nyota huyo ili kushtua dunia.
Ronaldo amebakiza miaka miwili kwenye mkataba wake
na bado hajasaini mkataba mpya. Tayari viongozi wa Manchester City
wamewasiliana na wakala wa Ronaldo, Jorge Mendes kwa ajili ya dili hilo.