Haruna Niyonzima (Pichani) amezidi kuupa presha uongozi wa Yanga kwa kuchelewa kujiunga na wachezaji wenzake walioko kambini, huku klabu hiyo ikidai amekuwa hapokei simu pale anapopigiwa.
Niyonzima aliondoka nchini kuelekea nyumbani kwao
Rwanda kwa ajili ya mapumziko baada ya msimu wa Ligi Kuu kumalizika,
lakini ameshindwa kuungana na wachezaji wenzake wa Yanga.
Awali, Kocha Mkuu wa Yanga, Ernest Brandts
alisema, mchezaji huyo aliomba aongezewe muda zaidi wa mapumziko akidai
ana matatizo ya kifamilia.
Hata hivyo, chanzo cha habari kutoka ndani ya
Yanga kimesema kuwa, uongozi wa klabu hiyo umechoshwa na
tabia ya mchezaji huyo ya kuomba “udhuru” kila anapokwenda mapumziko na
unaamini anafanya makusudi kuchelewa kujiunga na wenzake kutokana na
kujiona ana thamani zaidi ya wengine.
Chanzo hicho kiliendelea kusema kuwa, kibaya zaidi
Niyonzima amekuwa akilindwa na kocha wake Brandts hata pale anapokiuka
taratibu za klabu hiyo kutokana na kuwa na uhusiano naye mzuri.
“Nakwambia hapa tunavyoongea viongozi wakimpigia
simu hapokei na wakati mwingine anazima kabisa, kwa kweli jamaa
anawasumbua sana,” kilisema chanzo hicho na kuongeza:
“Kinachowaudhi zaidi viongozi na hata wachezaji
wenzake ni kwamba Niyonzima akichelewa mazoezi kocha Brandts hamkemei
anampa sababu za uongo ndiyo imetoka, lakini afanye mwingine aone,
viongozi wanataka sasa hatua zichukuliwe ili isionekane kuna upendeleo.”
Gazeti hili lilimtafuta Katibu Mkuu wa Yanga,
Lawrence Mwalusako ambaye alikiri kuwa amejaribu kumtafuta mara kadhaa
mchezaji huyo kupitia simu yake ya mkononi, lakini hakupokea jambo
ambalo linamshangaza.
“Nilimpigia simu sana jana (juzi Jumatano), lakini
hapokei sasa sijui ana tatizo gani na hatumuelewi kwa kweli,
tutaendelea kumtafuta,” alisema Mwalusako.
Naye Kocha Msaidizi wa Yanga, Fred Felix
alipotafutwa kuzungumzia suala hilo alisema, “Mimi nipo Tabora hayo
mambo ya Niyonzima wanaopaswa kuzungumzia wapo Dar es Salaam, wao ndiyo
wanajua lini anakuja au la.”
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa klabu hiyo,
Abdallah Bin Kleb aliwatoa wasiwasi mashabiki na wanachama wao kuwa wana
mawasiliano ya karibu na Niyonzima na kama angekuwa amepata timu, basi
wasingesita kutangaza mikakati yao.