KLABU ya Manchester United imeangushwa
katika mbio za kuwania saini ya kiungo wa kimataifa wa Hispania, Thiago
Alcantara baada ya mchezaji huyo kukubali kujiunga na Bayern Munich
akitokea Barcelona kwa dau la Pauni Milioni 22.
Kiungo huyo atasaini Mkataba wa miaka minne na mabingwa hao wa Ulaya na atakwenda kufanyiwa vipimo vya afya siku zijazo.
Dili hilo pia linahusisha makubaliano ya
klabu hizo mbili kucheza mechi ya kirafiki wakati fulani katika miaka
minne ijayo, wakati Thiago suala lake binafsi limepata mwafaka mzuri.
"Thiago Alcantara alikuwa kivutio kikuu
kwa kocha wetu mpya, Pep Guardiola,"amesema Mwenyekiti wa Bayern,
Karl-Heinz Rummenigge. "Tunayo furaha ya kufanikisha uhamisho mkubwa.
Thiago ametoka tu kuchaguliwa mchezaji bora wa michuano ya vijana ya
Mataifa ya Ulaya chini ya umri wa miaka 21. Ni mchezaji mzuri ambaye
ataongeza nguvu Bayern,".

Amekwenda: Thiago alikerwa na kutopewa nafasi ya kutosha Barcelona
Kiwango cha Thiago kimefanya azitoe mate
klabu kadhaa kubwa Ulaya, ikiwemo United, na Guardiola aliripotiwa
akisema kiungo huyo ni mchezaji nambari moja anayemtaka majira haya ya
joto.
Aling;ara na kuiwezesha Hispania kutwaa Kombe la Ulaya la U21, akifunga Hat-trick katika fainali dhidi ya Italia.

Mshindi: Thiago akisherehekea na taji la UEFA la U21
Alizaliwa Italia na wazazi Wabrazil,
kabla ya kujiunga na akademi ya Barcelona alikofundwa soka ya kitaalamu
hadi mwaka 2008 alipoanza kucheza.
Guardiola alimpandisha Thiago timu ya
kwanza misimu miwili iliyopita na alicheza mechi 45, lakini maumivu
yalimpunguzia idadi ya mechi hadi 36 msimu uliopita chini ya kocha Tito
Vilanova, Barcelona ikitwaa ubingwa wa Ligi ya Hispania.
Pamoja na kuchezesha timu vizuri, kuwa
na uwezo wa kupiga chenga na kufumua mashuti ya mbali, hakuweza kuwa
chaguo la kwanza katika safu ya kiungo ya Barcelona mbele ya akina
Andres Iniesta, Xavi Hernandez na Cesc Fabregas.