come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

MAZOEZI YA YANGA NOMA, MRISHO NGASSA AFUNIKA

Kiungo wa kimataifa Mnyarwanda Haruna Niyonzima ‘Fabregas’ wa Yanga jana hakuwapo kwenye Uwanja wa shule ya sekondari Loyola uliopo Mabibo, Dar es Salaam wakati kikosi cha klabu hiyo kilipoanza kujifua rasmi kujiandaa kwa msimu ujao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

Aidha, beki wa kati wa mabingwa hao wa Bara na timu ya taifa (Taifa Stars), Kelvin Yondani, Simon Msuva na kipa wao mpya Deogratius Munishi 'Dida', waliyemsajili akitokea Azam, hawakuwapo pia katika mazoezi hayo yaliyosimamiwa na kocha Mholanzi Ernie Brandts na msaidizi wake Felix Minziro.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa mazoezi hayo, Afisa Habari wa klabu hiyo, Baraka Kizuguto alisema wachezaji hao wanatarajiwa kurejea mazoezini leo.

“Tumepata taarifa zao lakini hatuwezi kuweka wazi matatizo yanayowakabili. Kesho (leo) wale ambao hawamo kwenye timu ya taifa (Taifa Stars), wataungana na wenzao mazoezini,” alisema Kizuguto.

Winga Mrisho Ngassa, ambaye msimu uliopita alikuwa Simba kwa mkopo akitokea Azam, ni miongoni mwa wachezaji walioanza mazoezi jana kujiandaa kwa ligi kuu na mashindano ya kimataifa ambapo Yanga itaiwakilisha Tanzania katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika.

Mshambuliaji Shaban Kondo aliyejiunga na Yanga kama mchezaji huru akitokea nchini Msumbiji, pia alifanya mazoezi jana yaliyohudhuriwa na wachezaji 13 tu.

Wachezaji waliofanya mazoezi jana ni: Alli Mustafa 'Barthez', Juma Abdul, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, David Luhende, Nadir Haroub 'Cannavaro', Salum Telela, Didier Kavumbagu, Jerson Tegete, Abdallah Mnguli, Nizar Khalfani, Frank Domayo, Ngasa na Kondo.

Minziro aliliambia gazeti hili baada ya mazoezi kuwa kikosi chao kinaendelea na mazoezi leo na kwamba Ijumaa kitasafiri kwenda jijini Mwanza kuanza ziara yao ya Kanda ya Ziwa kwa ajili ya kulitembeza kombe la ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara na kucheza mechi za kirafiki.

Mpaka sasa Yanga, ambayo bado haijatangaza rasmi wachezaji wake kwa ajili ya msimu ujao, ina kikosi chenye jumla ya wachezaji 19, ambao kwa sasa wameshasajiliwa kwa ajili ya msimu huo.

Msimu uliopita Yanga iikuwa na jumla ya wachezaji 27 walioipa ubingwa, lakini kwa sasa ina wachezaji 19, watatu Dida, Ngassa na Kondo wakiwa ni wachezaji wapya huku wachezaji 10 waliomaliza mikataba, wakinyimwa mikataba mipya.

Hata hivyo, kikosi cha Yanga kitalazimika kuwakosa Cannavaro, Yondani, Luhende, Msuva, Domayo, Barthez na Ngassa ambao leo wataungana na kikosi cha kocha Mdenmark Kim Poulsen katika kambi ya timu ya taifa (Taifa Stars) kujiandaa kwa mechi ya kuwania kufuzu Fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) dhidi ya Uganda.

Mechi hiyo itachezwa Julai 13 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na timu hizo zitarudiana wiki mbili baadaye jijini Kampala, Uganda.
Wakati huo huo, Somoe Ng'itu anaripoti kuwa, uongozi wa Yanga umeandika barua ya kuwahitaji nyota wake saba kutojiunga na kambi hiyo ili wasafiri nao kwenda jijini Mwanza.

Mabingwa hao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Yanga wanatarajia kucheza mechi ya kirafiki ya kimataifa Jumamosi dhidi ya timu ya KCC.

Akizungumza na gazeti hili jana, Afisa Habari wa Yanga, Baraka Kizuguto, alisema kuwa tayari wamewasilisha barua yao katika Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wakiwaombea ruhusa wachezaji wao lakini hadi jana mchana walikuwa hawajajulishwa chochote kuhusiana na maombi yao.