Baadhi ya wananchi wamekata tamaa kuhusu afya ya
shujaa wao huyo na wanapofika nje ya Hospitali ya Medclinic, Pretoria
alikolazwa, hushindwa kujizuia na kumwaga machozi. Baadhi yao wamekuwa
wakisema ‘wako tayari kwa taarifa mbaya’ kuhusu kiongozi huyo
aliyeongoza vita dhidi ya ubaguzi wa rangi.
Mandela (94) ambaye sasa anatajwa kwa jina la Tata
yaani Baba wa Taifa la Afrika Kusini, amelazwa katika hospitali hiyo ya
magonjwa ya moyo na hali yake inaelezwa kuwa ni mbaya huku taarifa
zikisema ‘anapumua kwa msaada wa mashine’.
Hali hiyo imewachanganya wananchi wa Afrika Kusini
akiwamo Rais Jacob Zuma na familia ya Mandela ambayo tayari imeingia
katika mgogoro mkubwa unaotafsiriwa na baadhi ya watu kwamba ni ‘kuwania
madaraka’ ikiwa kiongozi huyo atafariki dunia.
Usiku wa kuamkia Jumamosi, Mwenyekiti wa Taifa wa
Wanawake wa Chama tawala cha ANC, Baleka Mbete aliongoza maombi ya
kumwombea Mandela kwa wanachama na makada wake waliopo katika Majimbo ya
Cape Town na Eastern Cape huku akisisitiza: “Lazima wananchi wa Afrika
Kusini wafike mahali wamruhusu Mandela ampumzike kwa mapenzi ya Mungu.”
Ukubwa kwa kishindo cha ugonjwa wa Mandela
unaonekana hospitalini Medclinic alikolazwa, katika makazi yake Mtaa wa
Houghton, Barabara ya Laan 12, Johannesburg na makazi yake ya zamani
huko Soweto kwani maeneo hayo yamekuwa na harakati zisizokoma. Watu kwa
mamia, wamekuwa wakifika wakiwa wamebeba mabango, kadi, mishumaa na
maua, wengine katika makundi wakiimba, kusoma maneno ya Mungu na kufanya
sala.
Wapo wanaoifananisha hali iliyopo nje ya kuta za
Medclinic na Houghton na ukuta uliokuwa umezunguka jela alikokuwa
amefungwa katika Kisiwa cha Robben kwa miaka 18 kati ya 27 aliyokaa
gerezani.
“Kama watu walivyokuwa wakikaa nje ya kuta za
Gereza la Robben na kupaza sauti zao kwamba wanataka Mandela aachiwe
huru, ndivyo inavyoonekana leo. Watu wanapaza sauti, wanataka Mandela
kutoka ndani ya kuta za Medclinic,” anasema mmoja wa watu waliokuwa
kwenye lango la kuingia hospitalini hapo.
Kulia mwa lango hilo lililopo Mtaa wa Celliers,
kuna idadi kubwa ya kadi na mabango ambavyo vina ujumbe mbalimbali kwa
ajili ya Mandela, maua na mishumaa ambayo huwashwa na watu wanaofika
sehemu hiyo. Kutokana na hali hiyo, mtaa huo umefungwa pande zote mbili
kwa polisi kuweka vizuizi.
Jumamosi iliyopita, hofu juu ya afya ya Mandela
iliongezeka hasa baada ya kuwapo kwa pilika nyingi Houghton zilizodumu
kwa saa kadhaa, zikiwamo usafi usio wa kawaida uliojumuisha utengenezaji
wa bustani za maua, ufagiaji wa barabara na matengenezo ya njia za
umeme.
Mmoja wa majirani wa Mandela, Jacob Brews alisema harakati hizo si za kawaida na kwamba huenda ‘kuna jambo la ziada’.
Matukio hayo kwa jumla yake yamevivutia vyombo vya
habari vya Afrika Kusini na vya kimataifa ambavyo vimeweka kambi katika
maeneo hayo matatu yanayoonekana kuwa ni muhimu vikisubiri chochote
kitakachotokea.