Uwanja huo wa kisasa unaokidhi vigezo na mahitaji
ya kimataifa, ni wa kwanza na pekee kwa aina yake Afrika Mashariki na
Kati, ukiwa na uwezo wa kuingiza watazamaji 60,000. Umegharimu zaidi ya
Sh60 bilioni.
Ujenzi wa uwanja huo umekamilika baada ya miaka
saba kufikia siku ya kukabidhiwa jana, chini ya Kampuni ya Ujenzi
Beijing Construction Engineering Company (BCEC) Limited kutoka China.
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa uwanja huo
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Fenella Mukangara
aliishukuru China kwa kufanikisha ujenzi huo.
“Tunaishukuru China kwa mchango wake wa fedha,
kwani sasa tupo kwenye ramani ya dunia tukimiliki uwanja wa kisasa kiasi
hata kituo vya televisheni kimataifa, SuperSport kimekubali kututangaza
duniani kote,” alisema Mukangara.
Kwa upande wake, Balozi wa China nchini, Luo
Youging alisema ana matumaini makubwa kuwa Serikali itausimamia vizuri
uwanja huo kwa kukuza na kuendeleza vipaji katika michezo mbalimbali.
“Sasa vijana Watanzania watajenga afya zao kwani
uwanja huu unakidhi mahitaji yote muhimu ikiwemo soka na riadha. Pia
utatumika kuitangaza Tanzania duniani kote, alisema Youging.
Aidha, Waziri Mukangara alisema kuanzia sasa, Serikali itasimamia
kikamilifu mapato ya uwanja kufuatia malalamiko ya
mara kwa mara kuhusu uchache wa pesa kulinganisha na idadi ya mashabiki
wanaoingia.
“Tutadhibiti hali hii, tusingependa kuona
malalamiko haya yanakuwa hoja ya kila siku. Kama watu 15 wameingia
uwanjani, basi pesa za watu 15 zionekane,” alisema Mukungara.
Serikali imekabidhiwa uwanja huo baada ya miaka
miaka tangu ulipotumika mara ya kwanza mwaka 2007 kwa mchezo wa kirafiki
wa kimataifa dhidi ya timu ya Taifa Uganda, na kisha kufuatiwa na mechi
dhidi ya Msumbuji.