come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

YANGA KUCHUKUA MAMILIONI YAO LEO VODACOM

Wadhamini wa Ligi Kuu ya Tanzana Bara, kampuni ya huduma za simu ya Vodacom Tanzania wanakabidhi zawadi kwa mabingwa Yanga katika hafla maalum inayofanyika jijini Dar es Salaam leo jioni.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Soka (TFF), Wallace Karia alisema jumla ya Sh. milioni 200 zilizotolewa na kampuni hiyo kwa ajili ya zawadi kwa mabigwa (Yanga), wachezaji, marefa, kocha na timu yenye nidhamu.

Alisema Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara ndiye atakayekuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo itakayoanza saa 12:00 jioni.

“Tunatambua kwamba Yanga wametishia kutohudhuria hafla hiyo wakishinikiza tuwalipe fedha zao kwanza, lakini tutaendelea na timu na watu wengine watakaokuwapo,” alisema Karia.

Zawadi kwa mabingwa wa ligi hiyo imeongezeka kutoka Sh. milioni 50 za msimu wa 2011/12 hadi Sh. milioni 70 huku zawadi ya mfungaji bora itakayotua kwa Kipre Tcheche wa Azam ni Sh. milioni 5.

Mbali ya bingwa na mfungaji bora, Vodacom Tanzania pia itatoa fedha kwa timu ya Azam iliyomaliza katika nafasi ya pili, Simba iliyomaliza ya tatu na Kagera Sugar iliyomaliza ya nne katika msimamo wa ligi ambazo ni Sh. milioni 35, Sh. milioni 25 na Sh. milioni 20 zote zikiwa na ongezeko ikilinganishwa na zawadi za fedha zilizotolewa katika msimu wa 2011/12.

Zawadi nyingine zinazotolewa leo ni pamoja na zawadi ya Mchezaji Bora wa Mwaka na Kipa Bora, ambao kila mmoja atajinyakulia Sh. milioni 5.

Mwamuzi Bora na Kocha Bora kila mmoja atajipatia Sh. milioni 7.5 wakati timu yenye nidhamu itazawadiwa fedha taslimu Sh. milioni 15.

"Tumekuwa na msimu mzuri uliojaa ushindani na hamasa, tunatarajia timu zitajipanga zaidi kwa ajili ya msimu ujao na hivyo kuendelea kuipa ubora ligi yetu," alisema Salim Mwalim, Meneja wa Uhusiano wa Nje wa Vodacom Tanzania katika mahojiano na gazeti hili jana jijini Dar es Salaam.