come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

NIYONZIMA SASA KIMENUKA YANGA

BAADA ya kukataa ofa iliyotolewa na Klabu ya El Merreikh ya Sudan, uongozi wa Yanga sasa upo tayari kufanya mazungumzo na timu yoyote itakayomhitaji kiungo wake wa kimataifa raia wa Rwanda, Haruna Niyonzima (Pichani kulia), lakini kwa masharti.


El Merreikh kipindi cha usajili kilichopita, iliwasilisha maombi ya kumtaka kiungo huyo, lakini Yanga ilikataa kwa madai ofa iliyotolewa ni ndogo na kwamba thamani ya nyota huyo ni zaidi ya sh milioni 250.

Kutokana na kiwango hicho, timu hiyo ilishindwa na baadaye kuelekeza nguvu kwa aliyekuwa mshambuliaji wa Simba akicheza kwa mkopo kutoka Azam FC, Mrisho Ngassa, lakini mchezaji huyo akagoma.

Akizungumza jijini Dar es Salaam juzi, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga, alisema wapo tayari kumuachia Niyonzima kwa klabu ambayo itatoa dau nono litakaloendana na thamani ya kiungo huyo.

Alisema lazima taratibu zifuatwe, mbali na hiyo hawajapata timu yoyote inayommendea nyota huyo, lakini kama itatokea wapo tayari kukaa nao meza moja kuzungumza na kumuuza kwa dau ambalo Yanga itanufaika nalo.

Alisema soka ya sasa ni biashara na hakuna atakayetaka kumuuza mchezaji wake kwa hasara, lazima faida ya kutosha iwepo, ambayo itawasaidia kupata kiungo mwingine mwenye thamani kama ya Niyonzima.

Kiungo huyo anayetarajiwa kurejea nchini Julai 14, amekosa ziara ya timu yake iliyopo Kanda ya Ziwa kulitembeza kombe lao la ubingwa wa Bara walilotwaa pamoja na kuuza bidhaa zao.

Tayari ilicheza na KCC ya Uganda, ambapo mechi ya kwanza walitoka sare ya bao 1-1 huku marudiano wakifungwa 2-1 na jana walikuwa mjini Tabora kuumana na Rhino Rangers.