Mshambuliaji nyota Amissi Tambwe wa mabingwa wapya
wa mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la
Kagame), Vital'O na timu ya taifa ya Burundi alitua jijini Dar es Salaam
juzi usiku lakini usajili wake ulikwama kutokana na kutokuwapo kwa
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hanspoppe,
imefahamika.
Akizungumza jana, Katibu Mkuu wa Simba, Evodius Mtawala, alisema kwamba mazungumzo ya awali na mchezaji huyo yamekamilika na kinachosubiriwa sasa ni kusaniwa tu kwa mkataba huo.
Mtawala alisema kwamba mshambuliaji huyo amesharidhia kiasi cha fedha ambacho atapatiwa na wanatarajia kumpa mkataba wa miaka miwili kuichezea Simba.
"Tayari tuko naye na anayesubiriwa sasa ili kukamilisha zoezi hili ni Hanspope ambaye yuko nje ya nchi... lakini naye wakati wowote kuanzia leo (jana) atarejea nchini," alisema Mtawala.
Tambwe ndiye mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Burundi na katika mashindano ya Kombe la Kagame yaliyomalizika mapema mwezi huu, alifunga magoli sita na kuisaidia timu yake kutwaa ubingwa wa michuano hiyo kwa mara ya kwanza tangu Vital'O ilipoanza kushiriki mwaka 1994.
Mtawala aliongeza kuwa wanafahamu uwezo wa mshambuliaji huyo ambaye kabla ya kumshawishi atue klabuni kwao, tayari walishaangalia video za mechi mbalimbali alizocheza akiwa na timu ya taifa ya Burundi.
Tambwe anatarajiwa kuiongezea nguvu Simba katika safu ya ushambuliaji ambayo msimu uliopita ilionekana kupwaya wakati klabu hiyo iliposhindwa kutetea taji la Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwa kumaliza katika nafasi ya tatu na pia kutolewa katika hatua ya awali ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika baada ya kukubali kipigo cha jumla cha mabao 5-0 kutoka kwa Recreativo de Libolo ya Angola.
Wachezaji wengine wa kimataifa waliosajiliwa Simba hadi sasa ni Waganda Abel Dhaira ambaye ni kipa na beki kisiki, Samuel Senkoomi.
Hata hivyo, Dhaira bado hajajiunga na wachezaji wenzake ambao wanaendelea na maandalizi ya msimu ujao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara itakayoanza Agosti 24.
Katika hatua nyingine, Mtawala alisema kuwa kikosi cha timu yao kinachoongozwa na kocha Abdallah Kibaden 'King' kinatarajiwa kurejea jijini Dar es Salaam leo kikitokea mkoani Katavi ambapo jana jioni kilicheza mechi ya kirafiki dhidi ya wenyeji, timu ya kombaini ya mkoa huyo mpya.