Alisema hayo jana katika mitambo ya kufua umeme ya
Symbion na kubainisha kuwa Marekani imetenga kiasi cha Dola 7 bilioni
zitakazotolewa kwa nchi sita za Afrika katika kipindi cha miaka mitano
kugharimia miradi ya umeme.
Akizungumza mbele ya mwenyeji wake, Rais Jakaya
Kikwete, Rais Obama alisema utamaduni wa kuchelewesha utekelezaji wa
miradi haufai kufumbiwa macho kwani unakawiza maendeleo kwa wananchi
wenye shida.
“Utakuta mradi unakaa kwa miaka saba au minane
bila ya kutekelezwa, jambo hilo hatutaki litokee. Mara mradi unapopangwa
na mipango kukamilika, basi utekelezwe haraka iwezekanavyo ili wananchi
waone faida zake,” alisisitiza Rais Obama.
Rais Obama alikuwa akizungumzia mradi mkubwa wa
umeme unaofadhiliwa na nchi yake ujulikanao kama ‘Power Afrika’ ambao
pamoja na fedha hizo za Serikali yake, taasisi mbalimbali binafsi nazo
zimetoa Dola 9 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wake.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya hotuba
hiyo ya Rais Obama, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter
Muhongo alisema tatizo la ucheleweshaji wa miradi halipo kwa Tanzania
kwa kuwa Serikali imejipanga vyema kuhakikisha kuwa mambo yanakwenda kwa
kasi chini ya utaratibu mpya wa ‘Matokeo Makubwa Sasa’ (Big Results
Now) inayosimamiwa na Kitengo cha Ofisi ya Rais kinachoitwa President’s
Delivery Unit.
Hata hivyo, Profesa Muhongo alisema tayari
Tanzania imeshaorodhesha miradi ambayo ingependa itekelezwe chini ya
mpango huo na tayari miradi hiyo imeshawasilishwa katika ofisi za
Ubalozi wa Marekani nchini.
Waziri Muhongo alisema miradi mingi ni ya umeme vijijini ambayo inatekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (Rea).
Katika hotuba yake fupi, Rais Obama alibainisha
kuwa lengo la Marekani ni kuzisaidia nchi za Afrika kujiondoa katika
umasikini ili ziondokane na kuwa ombaomba wa misaada.
“Kwa yale niliyoyaona katika ziara yangu ya wiki
moja kuanzia Senegal, Afrika Kusini na hapa Tanzania, ni dhahiri kuwa
Afrika ina uwezo wa kujiondoa katika umasikini,” alisema Rais Obama.
Alisema mradi huo wa Power Africa unalenga mambo
mawili makubwa. Kwanza, kuhakikisha kuwa idadi ya watu wanaopata umeme
inaongezeka maradufu na pili kuziwezesha nchi za Afrika kujenga uwezo wa
kuzalisha umeme wa kutosha.
“Kwa kuanzia, ili kutekeleza dhamira hiyo,
tutahakikisha kuwa tunawapatia umeme watu milioni 20 katika nchi sita
ambako mradi huu utatekelezwa,” alisema.