TAIFA STARS WAINGIA KAMBINI LEO, TAYARI KUIUA UGANDA
TIMU
ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars inatarajiwa kuingia kambini
leo katika hoteli ya Tansoma, Dar es Salaam kujiandaa na mechi dhidi ya
Uganda, The Cranes kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika kwa
Wachezaji wa Ligi za Ndani (CHAN) zitakazofanyika mwakani nchini Afrika
Kusini.
Wachezaji
walioteuliwa na Kocha Mdenmark, Kim Poulsen katika kikosi hicho ni
David Luhende (Yanga SC), Aggrey Morris (Azam), Aishi Manula (Azam),
Ally Mustafa (Yanga), Amri Kiemba (Simba), Athuman Idd (Yanga), Frank
Domayo (Yanga), Haroun Chanongo (Simba), John Bocco (Azam), Juma Kaseja
(Simba), Juma Luizio (Mtibwa Sugar) na Kelvin Yondani (Yanga).
Wengine
ni Khamis Mcha (Azam), Mrisho Ngasa (Simba), Mudathiri Yahya (Azam),
Mwadini Ali (Azam), Mwinyi Kazimoto (Simba), Nadir Haroub (Yanga), Salum
Abubakar (Azam), Shomari Kapombe (Simba), Simon Msuva (Yanga) na
Vincent Barnabas (Mtibwa Sugar).
Taifa
Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itacheza na Uganda
Julai 13 mwaka huu, saa 9:00 Alasiri kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam kabla ya kurudiana wiki mbili baadaye mjini Kampala, Uganda.
Kim
anatarajiwa kutumia mechi hizo za kufuzu CHAN kuwapoza machungu
Watanzania, baada ya kupoteza nafasi ya kwenda katika Fainali za Kombe
la Dunia Brazil mwakani, kufuatia kufungwa mabao 4-2 na Ivory Coast
katika mchezo wa Kundi C mwezi uliopita Dar es Salaam.
Makamu
Mwenyekiti wa Yanga SC, Clement Sanga jana amewaondoa hofu wapenzi wa
soka nchini kuhusu wachezaji wa timu yake walioitwa kwenye kikosi cha
Stars.
Kulikuwa
kuna habari kwamba, Yanga ambayo itaondoka Julai 5 Dar es Salaam kwenda
kanda ya Ziwa kwa ziara ya wiki moja, haitaruhusu wachezaji wake
kujiunga na kambi ya Stars, lakini Sanga jana amesema wataripoti timu ya
taifa leo.