Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amesema kikosi cha Taifa Stars sasa kina uwezo wa kushindana katika mashindano yoyote, kwani tayari kimeiva.
Akizungumza na wachezaji wa timu hiyo kambini kwao hoteli ya Tansoma, Dar es Salaam, Rais Tenga aliwaambia kuwa kiwango walichoonesha kwenye mechi zilizopita za mchujo za Kombe la Dunia dhidi ya Morocco na Ivory Coast kimethibitisha hilo.
“Kiwango mlichoonyesha katika mechi hizo kila Mtanzania anayewafuatilia amekiona, hivyo hatuna shaka kuwa mtatuwakilisha vizuri kwenye mechi ya kesho dhidi ya Uganda,” amesema Rais Tenga na kuwataka kupigana kwa ajili ya Tanzania.