come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

WARUNDI KUAMUA HATIMA YA STARS NA UGANDA



Wakati Shirikisho la Soka Afrika (Caf) likiwateua waamuzi kutoka Burundi kuchezesha mechi ya kwanza ya mchujo kuwania kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (Chan) kati ya Tanzania na Uganda, Fifa imefuta mechi ya kirafiki ya maandalizi ya mchezo huo kati ya The Cranes na Timu ya Taifa ya Iran.
Fifa, Shirikisho la Kimataifa la Soka Ulimwenguni, imefuta mchezo huo wa kirafiki wa kimataifa uliopangwa kuchezwa nchini Iraq Jumanne wiki ijayo kwenye Uwanja wa Erbil City kwa sababu za kiusalama.
Mechi hiyo ilipangwa kuchezwa Jumanne wiki ijayo kwenye Uwanja wa Erbil City ambao umefungiwa na Fifa kwa muda usiojulikana kutokana na shambulio la bomu.
Uganda iliomba kucheza mchezo huo kama sehemu ya maandalizi kabla ya kuja Tanzania kucheza na Taifa Stars wiki ijayo, ambapo timu itakayoibuka na ushindi katika mechi ya nyumbani na ugenini itafuzu (Chan).
Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka la Uganda (Fufa), Mujib Kasule alithibitisha jana taarifa za Fifa kuupiga ‘stop’ mchezo huo na kuagizwa uchezwe nchi nyingine.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Boniface Wambura aliwataja waamuzi hao kuwa ni Thierry Nkurunziza atakayepuliza filimbi, wakati wasaidizi wake watakuwa Jean Claude Birumushahu na Pascal Ndimunzigo.
Pia alimtaja mwamuzi ambaye pia ni Mrundi kuwa ni Pacifique Ndabihawenimana. Wambura alisema, kamishna wa mchezo huo atakuwa Gebreyesus Tesfaye kutoka Eritrea, ambaye ni Mwenyekiti wa Chama Soka Eritrea na mjumbe wa Kamati ya Maandalizi ya Mashindano ya Chan.
Katika hatua nyingine, Wambura alisema Caf imeteua Mtanzania Leslie Liunda kuwa Kamishina wa mechi kati ya Burundi na Sudan itakayopigwa Bujumbura.