Yanga walikuwa wa kwanza kufunga bao kupitia kwa
Hamis Thabiti, kisha KCC wakasawazisha kwa bao la ‘jioni’ kupitia kwa
mshambuliaji Kavuma Willy.
Katika mchezo huo, ulioshuhudia Yanga ikitawala
zaidi kipindi cha kwanza na KCC kipindi cha pili, ulijaa kosakosa nyingi
za mabao kutoka kila upande.
Wenyeji Yanga waliokuwa wakicheza mchezo wa kwanza
wa kirafiki wa kimataifa baada ya kusajili wachezaji kadhaa, walikuwa
wa kwanza kufanya shambulizi langoni kwa KCC, lakini likaishia kwa Juma
Abdul kupiga shuti lililokosa shabaha kutokana na pasi ya Abdallah
Mguli.
Nizar Khalfan angeweza kufunga muda mfupi baadaye
kama siyo kupiga mpira wa adhabu ndogo nje ya lango la Waganda hao
kutokana na mpira wa adhabu ndogo.
Yanga waliocheza kwa kuonana vizuri nusu ya
kipindi cha kwanza, walishindwa tena kutikisa nyavu za KCC, na safari
hii ilikuwa zamu ya beki Mbuyu Twite aliyeshindwa kuusukumia kwenye
kamba mpira wa kona iliyochongwa na Salim Telela katika dakika ya 19.
KCC walijipanga na kujibu mashambulizi, ambapo
kipa wa Yanga Deo Mushi alifanya kazi nzuri kulicheza shuti la mwendo
mrefu lililopigwa na Kavuma Willy katika dakika ya 32.
Baada ya kosakosa nyingi, Yanga waliandika bao la
kwanza likifungwa na Hamis Thabiti katika dakika ya 40 kwa kiki kali
iliyomshinda kipa wa KCC, Francis Oginga.
Wageni KCC, wangeweza kusawazisha bao hilo kama
wangetumia vizuri nafasi mbili katika dakika za 72 na 74, lakini
washambuliaji wake, Kavuma Willy na mtokea benchi Semanda walipiga
mipira nje.
Katika dakika ya 89, KCC walisawazisha bao hilo
kwa kiki ya adhabu ndogo iliyokwenda moja kwa moja kugusa nyavu za Yanga
na kumwacha Mushi asijue la kufanya.