Na Fikiri Salum
HII ndio bongo! mambo yanaendeshwa kiujanjaujanja, unaweza kushangaa uteuzi wa timu ya taifa kusikia mchezaji aliyeshushwa kikosi cha pili cha timu fulani lakini akawemo katika kikosi cha Taifa Stars kinachocheza mechi ngumu ya kimataifa.
Ukiendelea kushangaa hilo unakutana na hili, Shadrack Nsajigwa na Gofrey Bonny ni wazee na wameacha kucheza soka, lakini wanaibukia Nepal na kuwa katika kikosi cha kwanza katika moja ya vilabu vinavyoshiriki ligi kuu nchini humo.
Jana shirikisho la kandanda nchini TFF kupitia kamati yake ya sheria, hadhi za wachezaji ilipotangaza kupitia upya usajili wa mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda Emmanuel Okwi, Kamati hiyo ilitangaza kutengua usajili wake na kudai haijaridhishwa na maamuzi ya klabu ya Yanga kumtumia nyota huyo hivyo basi mpaka ipate mwongozo kutoka FIFA.
Kana kwamba haitoshi TFF ilisema kwamba Okwi hawezi kuichezea Yanga mpaka pale FIFA itakapomaliza kesi yake na klabu ya Etoile Du Sahel ya Tunisia, Yanga haijatoa tamko lolote tangia kutolewa maamuzi hayo ambayo yameteka hisia kwa sasa.
Isitoshe michuano ya ligi kuu inatarajia kuanza mwishoni mwa wiki hii, mashabiki wa soka nchini hasa wale wa Yanga wote wameinamisha shingo zao chini huku wale wa Simba wakifurahia, wanaiona TFF kama mwokozi wao, walishindwa kuficha sura zao pale Okwi alipotangazwa kusajiliwa na Yanga.
Hivyo sasa wanaiona TFF kama mkombozi wao, mashabiki wa Yanga vichwa chini, hawaamini kilichotokea, Na wale matajiri wao nao hoi, wametumia mamilioni ya fedha kuhakikisha Okwi anatua Jangwania, huenda fedha hizo zingewatosha katika mchakato wao wa kujenga uwanja wa mazoezi.
Timu yao hadi sasa inahaha kukodisha viwanja vya kufanyia mazoezi, mara Bora Kijitonyama au Loyola Mabibo, Timu yao karibu wiki mbili ilikuwa ziarani Uturuki kujiandaa na ligi kuu pamoja na michuano ya kimataifa, ambapo Yanga itashiriki klabu bingwa Afrika na itakuwa na kibarua rahisi pale itakapocheza na klabu ya Komorozine ya omoro.
Kwanini nasema TFF IMEVURUNDA KWA OKWI, ni kwa sababu tayari muda wa usajili umekwisha na ligi inatarajia kuanza siku tatu kabla ya kutangazwa taarifa hiyo, ni kama wameikomoa Yanga, sikubaliani hata kidogo na maamuzi hayo na ndio maana nafikia kuandika makala hii.
Kwanza sijaridhishwa na wajumbe wa kamati mbalimbali wa TFF, Wengi wao ni Yanga na Simba, wanatoka katika vilabu hivyo na wala hawajui maana halisi ya soka, zaidi kukomoana, na wale waliotoka Yanga wanatokana na makundi yaliyoshindwa katika uchaguzi mkuu wa klabu ya Yanga.
Wanaikomoa timu yao aidha kwa sababu binafsi tu ama hawampendi mtu fulani pale, Kamati haijatenda haki kwa Yanga pia kwa mchezaji husika, Etoile Du Sahel walikuwa wapi muda wote hadi wakurupuke sasa na kupmtangaza kuwa Okwi ni mali yao wakati hawajamlipa mshahara wame wa miezi mitatu sasa.
Etoile Du Sahel bado hawajapewa dhamana ya kumtumia mchezaji huyo ambaye aliidhinishwa na FIFA kuichezea SC Villa ya Uganda kwa miezi sita tu, Makubaliano ya FIFA na FUFA shirikisho la kandanda nchini Uganda kwamba Okwi ataichezea SC Villa kwa miezi sita kisha atakuwa huru na timu yoyote itakayomuhitaji inaweza kumchukua.
Haijatajwa klabu gani inayoweza kumnunua Okwi, iwe Simba, Yanga, Azam au Etoile yenyewe kama inamuhitaji tena, TFF nayo ilikuwa wapi ilipoona Okwi anaruhusiwa kuichezea SC Villa kwa miezi sita, mbona walikuwa kimya! ina maana Okwi ruksa kuichezea SC Villa na si Yanga?
Okwi ni halali kabisa kwa Yanga, kilichotokea TFF ni ubabaishaji wao na kuweka maslahi ya Simba mbele, namnukuu rais wa TFF Jamal Malinzi pale alipothubutu kusema kuwa ataisaidia Simba katika sakata la Okwi, Malinzi alidai wanasimba wasiwe na wasiwasi kuhusu hilo.
Kweli amewasaidia, Malinzi ameishawishi kamati yake kumsimamisha Okwi kuichezea Yanga na badala yake atasota bila kucheza, FIFA hawataki kabisa mambo hayo, hawataki mchezaji akae nje ya uwanja kwa sababu ya matatizo na klabu yake, ndio maana walimruhusu aende SC Villa ya ganda ili kunusuru kiwango chake.
Yanga ilitumia kigezo cha kumsajili Okwi kulingana ruhusa ya FIFA kwa FUFA, ile ya kusema ataichezea SC Villa miezi sita kisha atakuwa huru, ilichokifanya Yanga ni kuinunua ile miezi sita ya SC Villa pia kuongeza miaka miwili inayotokana na ruhusa ya kuwa mchezaji huru mara tu atakapomaliza mkataba wake wa miezi sita katika klabu ya SC Villa.
Liko wapi kosa la Yanga? umefika wakati sasa viongozi wa soka mkae chini na kutafakari upya matatizo ya namna hii, lakini kwa upande mwingine Wanayanga nao wanapaswa kuchekecha vichwa vyao na kutuliza akili wakati wanapofanya maamuzi yoyote aidha ya usajili au kuvunja mikataba, usajili wa Okwi uligubikwa na utata tangia aliporuhusiwa kwenda kuichezea SC Villa mwishoni mwa mwaka jana.
Mbali na hilo nalikumbusha shirikisho letu la kandanda nchini kutenda haki kwa wanachama wake ambao ni vilabu, tayari wameivuruga Yanga ambao ni wawakilishi wetu katika michuano ya kimataifa, Yanga na Azam zitaiwakilisha Tanzania katika michuano ya vilabu ya kimataifa ambapo zimefanya maandalizi ya kutosha ili kushiriki vema michuano hiyo.
Azam ilikuwa katika maandalizi yake visiwani Zanzibar ambapo ilikwenda kushiriki michuano ya Mapinduzi Cup ambapo hata hivyo timu hiyo ilitolewa katika hatua ya nusu fainali, wakati Azam ikishiriki michuano hiyo ya Mapinduzi, Yanga ilikwenda nchini Uturuki.
Yanga itashiriki klabu bingwa Afrika, wakati Azam itashiriki michuano ya Shirikisho, maandalizi ya timu hizo mbili yanaonekana ya kuridhisha ambapo sasa ni dua tu za Watanzania zinahitajika, uamuzi wa TFF ni kama wanaisurubu Yanga ambayo iliamua kumsajili Okwi kwa lengo la kushindana katika michuano hiyo.
Endapo Yanga itavuka raundi ya awali basi inaweza kukutana na timu ngumu na bingwa mtetezi wa klabu bingwa Afrika Natioanl Al Ahly ya Misri, timu hiyo ya kutoka ukanda wa Kaskazini mwa Afrika imekuwa na ushindani mkubwa inapokutana na timu za Afrika mashariki.
Ushauri wangu kwa TFF isifanye mambo yake kishabiki wala kwa kukurupuka, ilipaswa kufuatilia mapema usajili wa Okwi FIFA na kujiridhisha mapema, sidhani kama kungetokea malalamiko ama hasara kwa Yanga, lakini kilichotokea sasa nadhani Wanayanga wataamini maneno ya Malinzi yamelenga kuikomoa timu yao na si kupata muafaka.