Serikali ya Tanzania imeipatia klabu ya Yanga ndege kwa ajili ya usafiri wa kwenda Zimbabwe kucheza mechi ya marudiano ya kombe la vilabu la Shirikisho barani Afrika dhidi ya wenyeji, Platinum FC.
Awali, Yanga ilipanga kuondoka leo lakini kwa mujibu wa katibu mkuu wa Yanga, Jonas Tibohora, wameahirisha safari yao mpaka Ijumaa baada ya serikali kukubali kuwapa ndege itakayowapeleka moja kwa moja Bulawayo.
“Tuliiomba Serikali kutupatia ndege ambayo tutaigharamia wenyewe kwenda Bulawayo”.
“Ndege ya Serikali imetuondolea usumbufu wa kuunganisha ndege kutoka Dar es Salaam mpaka Harare, Harare kwenda Bulawayo, kwa hiyo ndege yetu itaenda moja kwa moja mpaka Bulawayo na kuwaondolea uchovu wachezaji wa safari ndefu”, amesema Tibohora.
Hata hivyo, Yanga italazimika kuigharamia hiyo safari kwa pesa zake huku Serikali ikitoa tu chombo hicho cha kusafiria.
Yanga itacheza na Platinum wikiendi huku ikiwa na mseti wa magoli 5-1 waliyoyapata katika mechi ya awali iliyofanyika Dar es Salaam wiki mbili zilizopita.
Endapo wana Jangwani hao watafuzu kuitoa Platinum, huenda wakakutana na vigogo wa Afrika, Etoile du Sahel ya Tunisia katika hatua ngumu inayofuata.