Kocha mpya wa Taifa Stars, Boniface Mkwasa ametangaza benchi zito la ufundi linalojumuisha wachezaji maarufu wa zamani, Peter Manyika anayekuwa kocha wa makipa, Hussein Sued akiwa mtunza vifaa, Abdallah Kibaden anayekuwa mshauri mkuu na Juma Mgunda akiwa meneja.
Uteuzi wa wakongwe hao waliotamba kwa nyakati tofauti katika medani ya soka nchini unaonyesha dhamira ya kocha huyo wa Yanga kuibadili Stars na pengine kuirejeshea imani machoni mwa wapenzi wa soka nchini.
Pia, yumo mjumbe wa kamati ya utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Ahmed Mgoyi atakayekuwa mratibu.
Akizungumza na wanahabari jana jijini Dar es Salaam, Mkwasa alisema benchi la ufundi la Stars limeweka utaratibu wa kukutana na makocha wa klabu za Ligi Kuu na kushauriana nao masuala mbalimbali ya kiufundi yatakayokuwa na msaada kwa klabu na Taifa Stars.
Aliwataka mashabiki wa soka nchini kuliunga mkono benchi hilo jipya la ufundi kwani bila ushirikiano wao, yeye na wenzake hawawezi kufanya miujiza ndani ya timu hiyo.
“Mashabiki wanatakiwa kuiunga mkono timu ili mimi na wenzangu tupate nguvu ya kutimiza kile wanachokihitaji. Kama wakiendelea kurusha mawe au kuwatukana wachezaji wasitarajie kama tutafanikiwa,” alisema.
Mkwasa aliyekabidhiwa jukumu la kuinoa Stars juzi aliwataka Watanzania kuiunga mkono huku akitamba kuleta mabadiliko makubwa ya kiutendaji na kimfumo ndani ya timu hiyo.
Alisema kuwa yeye na benchi lake la ufundi wanafahamu kiu na matamanio ya Watanzania kwa timu hiyo, hivyo watajitahidi kuhakikisha wanawapa raha kwa kufanya vizuri kwenye michuano mbalimbali inayowakabili.
Kwa kuanzia, Mkwasa alisema kuwa wameweka utaratibu wa kuhakikisha mchezaji yeyote anayechaguliwa ndani ya kikosi hicho, ni lazima awe na namba kwenye kikosi cha kwanza kwenye klabu yake, sanjari na nidhamu ya hali ya juu.
“Ni lazima mchezaji anayechaguliwa kuiwakilisha nchi atambue kuwa anabeba dhamana ya Watanzania wenzake zaidi ya milioni 45, hivyo anatakiwa awe alama nzuri ndani na nje ya timu. Hatutomvumilia mchezaji asiyejitambua,” alisema.
Julio aunga mkono
Akizungumzia uteuzi wa benchi la ufundi Stars, kocha mkuu wa Mwadui, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ alisema ana imani timu hiyo itafanya kazi yake vizuri.