Mbali ya maofisa hao, pia jeshi hilo limemwondoa 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) 
Linus Sinzumwa, naye ikiwa ni miezi michache baada ya kutokea kwa ghasia
 wakati baadhi ya wakazi wa huko walipokuwa wakipinga mpango wa Serikali
 wa ujenzi wa bomba la gesi kwenda Dar es Salaam.
Nafasi ya Kamanda Sinzumwa imechukuliwa na 
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Zelothe Stephen kutoka 
Makao Makuu ya Polisi.
Taarifa iliyotolewa jana na Msemaji wa Jeshi la 
Polisi, Advera Senso ilisema Mkuu wa jeshi hilo, Inspekta Jenerali 
(IGP), Said Mwema amemteua, ACP Selemani Hamisi kuchukua nafasi ya Kato 
ambaye anahamishiwa makao makuu ya jeshi hilo. Kabla ya uteuzi huo, 
Kamanda Hamisi alikuwa Makao Makuu Idara ya Upelelezi.
IGP Mwema pia amemteua Mrakibu Mwandamizi wa 
Polisi (SSP) Hamad Hamad kuchukua nafasi ya Mwafwimbo aliyehamishiwa 
mkoani Lindi kuwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Lindi (OCD).
Taarifa hiyo ya Polisi ilisema uhamisho huo ni wa 
kawaida kwa mujibu wa kanuni, taratibu na miongozo yake. Hata hivyo, 
katika siku za karibuni, kumekuwa na malalamiko mengi kuwa vyombo vya 
usalama katika uwanja huo vimeshindwa kudhibiti biashara hiyo na matokeo
 yake Tanzania imechafuka katika medani ya kimataifa kutokana na idadi 
kubwa ya vijana wake kukamatwa sehemu mbalimbali duniani.
Matukio ya karibuni yanahusisha kukamatwa kwa 
wasanii Agnes Masongange na Melisa Edward waliokamatwa katika Uwanja wa 
Ndege wa Kimataifa wa Oliver Tambo, Johannesburg, Afrika Kusini.
Kutokana na kashfa hiyo, Waziri wa Uchukuzi, Dk 
Harrison Mwakyembe aliamua kulivalia njuga suala hilo na kuchukua hatua 
kadhaa na pia alifichua jinsi wasichana hao walivyosaidiwa kupitisha 
dawa hizo na mtandao uliohusisha polisi, maofisa usalama wa taifa na 
baadhi ya wafanyakazi wa JNIA.
RPC Mtwara
Sinzumwa anaondoka Mtwara baada ya ghasia kubwa 
zilizozuka Mei mwaka huu wakati baadhi ya wakazi wa Mtwara walipokuwa 
wakipinga gesi kutoka Msimbati kusafirishwa kwa bomba hadi Dar es 
Salaam.
Katika ghasia hizo, ambazo Jeshi la Wananchi 
Tanzania (JWTZ), liliingilia kati, polisi walishutumiwa na wakazi wa 
huko kwa kutumia nguvu kubwa na kuwasababishia madhara.
