Wakati Serikali ikisema Katiba ya Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF), ina upungufu na inapaswa kufanyiwa marekebisho, Mwanasheria
mkongwe na Mjumbe wa kudumu wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) Said El
Maamry, amemshauri msajili aipitishe katiba hiyo.
El Maamry amesema njia pekee ya kunusuru soka la
Tanzania kwa sasa ni kutoangalia nyuma upungufu mdogo kwenye katiba ya
TFF, kinyume na hapo ni kukaribisha mgogoro.
Juzi, Naibu Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo,
Amos Makala alikosoa uamuzi wa Rais wa TFF, Leodegar Tenga kutangaza
Kamati za Shirikisho hilo kabla ya Msajili wa Vyama vya Michezo
kuipitisha katiba ya TFF iliyofanyiwa marekebisho.
Makala alikwenda mbali na kutamka kuwa, kamati
hizo za TFF ni batili na kwamba uhalali wake utatimia tu iwapo Msajili
atayapitisha marekebisho ya katiba ya TFF.
“Katika marekebisho walitakiwa wanyooshe vidole
ijulikane wangapi wanasema ndio na wangapi wanakataa, lakini haikuwa
hivyo. Hapo hakuna katiba, wafanye jitihada kujinusuru, wafanye
utaratibu waitishe mkutano mwingine wa marekebisho ya katiba yao,”
alisema Makala.
TFF ilitakiwa kufanya marekebisho kwenye katika
kufuatia ushauri waliopewa na ujumbe wa Shirikisho la Soka Ulimwenguni
(Fifa) waliokuja nchini Aprili mwaka huu.
El Maamry aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa FAT enzi
hizo, alisema ingawa kuna upungufu mdogo, haoni kama ni jambo la busara
kuirudisha katiba hiyo kwani kuitisha mkutano mwingine wa dharura ni
gharama na kunaweza kuibuka mgogoro.
El Maamry alisema, msajili anachotakiwa kufanyia
kazi ni vipengele vilivyofanyiwa marekebisho na kuwasilishwa kwake
lakini siyo katiba nzima.
Akifafanua alisema: “Kama chama ni kipya msajili
anatakiwa kuangalia katiba nzima na kuipitisha, lakini kwa chama ni cha
muda mrefu kama TFF kinapopeleka mabadiliko anachotakiwa kuangalia ni
vile vipengele tu.”
Kuhusu kuundwa kwa kamati, El Maamry alisema Tenga
yuko sahihi kama kifungu kinachompa mamlaka kama Rais kufanya uteuzi
hakikuguswa kwenye mabadiliko, kinyume cha hapo ndiyo kamati zinaweza
kuwa batili.
El Maamry alisema ni vizuri msajili akatumia
busara kupitisha katiba hiyo pamoja na upungufu mdogo uliojitokeza kwa
lengo la kunusuru soka la Tanzania.
Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah, alisema
katikati ya wiki hii kuwa shirikisho halina taarifa za kuwepo na
upungufu kwenye katiba yao kama ilivyoelezwa na Waziri Makala.