Sakata la Yanga(Wakiwa pichani) kugomea udhamini wa Azam Tv limechukua sura mpya baada ya klabu hiyo kutaka kupewa kitita cha Sh600 milioni ili kukubali kudhaminiwa na Azam.
Habari za uhakika ambazo tumezipata
zinadai kuwa, Yanga wamepata kiburi cha kugomea udhamini wa Azam baada
ya kuwa na ofa mbili mkononi ya Pepsi na ile ya Zuku.
“Pepsi wanatoa kinywaji chao kipya Pepsi Cola na
wametupa ofa ya Sh600 milioni, Azam walifuatwa na kuelezwa juu ya ofa
hiyo wakakataa Pepsi wasiingie kwa vile ni wapinzani wao kwa Azam Cola,”
kilisema chanzo cha habari.
Chanzo hicho kilisema kuwa, Yanga waliwapa sharti
Azam la kuongeza dau kutoka Sh100 milioni na kama isingewezekana basi
waingie mkataba na Kampuni ya Pepsi.
“Hiki ni kinywaji cha Pepsi ni kipya na wanataka
kukitangaza kupitia Yanga, Zuku nao wametupa ofa ya Sh400 milioni,
kilichopo hapa ni mgongano wa kimasilahi,” kiliongeza chanzo hicho.
Inadaiwa kuwa, Azam wameingia kwenye ligi kwa
sababu wanataka kuuza ving’amuzi vyao, lakini dau walilotoa la Sh100 ni
dogo ingawa klabu nyingine ikiwemo Simba wamekubali.
Hata hivyo, Yanga kila kukicha imekuwa ikija na
madai tofauti na tayari wameshaweka msimamo wao ikiwa ni pamoja na
kuwahamasisha wanachama wao kupinga suala la udhamini wa Azam.
Klabu hiyo ya mtaa wa Jangwani imekuwa kila
kukicha ikitoa madai mapya ya kusisitiza kugomea udhamini huo wa Azam na
mapema wiki hii walisema wanagomea kwa vile kuna kipengele cha CD za
mchezo ambazo Azam ndiyo watazimiliki na kwamba wasingekuwa na shida na
mkataba wa Azam kama kampuni hiyo isingekuwa na timu kwani kitendo cha
kumiliki CD kuna uwezekano wa kuididimiza timu yao.
Hata hivyo Mwenyekiti wa Kamati ya Ligi, Wallace
Karia akizungumzia suala hilo alisema madai hayo ya Yanga hayana mashiko
kwani klabu zote zinapewa CD za kila mchezo, pia suala la TBL Yanga
siyo peke yao ambao wanadhaminiwa na TBL, kwani hata Simba nao ni
wadhamini wao na wamekubaliana na mkataba huo wa Azam.