Klabu ya Tottenham huenda
ikalazimika kumpiga faini nyota wake anayesakwa na Real Madrid, Gareth
Bale baada ya kukosa kufika uwanja wa mazoezi kwa siku ya pili
mfululizo.
Kocha wa Tottenham Andre Villas-Boas amesema Bale ni sharti kutimiza wajibu wake licha ya kuwa huenda akajiunga na Real Madrid.
Mabingwa hao wa Uhispania wametangaza azma yao ya kumsajili mchezaji huyo kwa kitita cha pauni milioni themanini na sita, kiasi ambacho ndicho kubwa zaidi duniani kwa klabu yoyote kumnunua mchezaji mmoja.
Bale, mweye umri wa miaka ishirini na minne, alitarajiwa kurejea kambini siku ya Jumanne baada ya timu hiyo kwenda likizoni katika eneo la Marbella.
''Kwa sasa Real inataka kumsajili Bale, ikiwa hilo litatokea tunamtakia kila la heri, lakini kwa kuwa hajafika kambini, hilo ni kosa na sharti airekebishe'' Alisema Villas-Boas.
Bale amehusishwa na klabu ya Real na kocha huyo wa Tottenham anasema usajili huo huenda ukakamilika hivi karibuni.
Klabu ya Tottenham haitaki kumuuza mchezaji huyo hadi pale watakapomsajili atakayechukua nafasi yake.
Ripoti zinasema Tottenham huenda ikamsajili mshambulizi wa klabu ya Roma kutoka Argentina Erik Lamela kuchukua mahala pa Bale.
Bale hajaichezea klabu ya Tottenham au timu ya taifa ya Wales msimu huu kutokana na Jeraha, lakini mapema siku ya Jumatano alitajwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Wales itakayocheza mechi ya kufuzu ya kombe la dunia dhidi ya Macedonia na Serbia baadaye mwezi huu.