Na Fikiri Salum
Kama walivyotoa ahadi ya mabao kwenye mchezo wa ligi kuu bara kati yao na Ruvu Shooting ambapo wachezaji wa Yanga waliahidi kuifunga magoli mengi timu hiyo, ndivyo itakavyokuwa katika mchezo wa klabu bingwa barani Afrika kati ya mabingwa wa Tanzania bara na wawakilishi pekee katika michuano ya kimataifa Yanga dhidi ya mabingwa watetezi wa Afrika Al Ahly ya Misri.
Yanga na Al Ahly ya Misri zitakutana Jumamosi ijayo kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ambapo wachezaji wa mabingwa hao wa bara wameahidi kuishushia kichapo kitakatifu Al Ahly kama waliofanyia Komorozine ya Comoro.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Emmanuel Okwi raia wa Uganda amesema ana usongo mkubwa katika michuano ya kimataifa na hasa mechi iliyo mbele yake, Okwi ametamba kutoka na magoli si zaidi ya mawili katika mechi hiyo kwani wapinzani wao ni timu ya kawaida kama nyingine, Naye Simon Msuva amedai Al Ahly ni timu ya kawaida na inafungika.
'Katika mchezo huo lengo langu ni kupeleka mashambulizi mengi langoni mwao na ikiwezekana na mimi nifunge moja au mawili, nawaambia mashabiki wa Yanga waje washuhudie kalamu ya magoli uwanja wa Taifa', alisema Msuva ambaye amekuwa katiika kiwango cha juu siku za hivi karibuni.
Mrisho Ngasa ambaye anaongoza kwa magoli barani Afrika ametamba kutoka na goli zake mbili ama tatu katika mchezo huo huku akiahidi mvua ya magoli kuendelea, 'Tutashinda tu katika mechi hiyo, Yanga hii si timu ya kuichezea ni moto wa kuotea mbali tena tutafunga mengi, ni msimu wetu kusonga mbele', alisisitiza Ngasa.
Kocha msaidizi wa Yanga Charles Boniface Mkwasa amesema Al Ahly ni timu ya kawaida sana na ameiona ilipocheza na Sfaxien katika fainali ya Super Cup, 'Ni timu ya kawaida na inawezekana tukaifunga, kuhusu goli ngapi hiyo ni mipango ya mungu lakini lazima tuwafunge, nimezijua mbinu zao na tutazifanyia kazi', aliongeza Mkwasa.