Wajumbe watatu wa Bunge la Katiba ambao ni wabunge wa CCM wametofautiana na msimamo wa chama chao kwa kuunga mkono kura ya siri itumike kuamua ibara za Rasimu ya Katiba.
Hilo lilitokea jana katika mjadala mkali baina ya wajumbe kuhusu ama matumizi ya kura za siri yatumike au kura za wazi.
Katika mjadala huo ulioonyesha mgawanyiko wa wazi, wajumbe wengi wanaotokana CCM na ambao wamekuwa wakipigania kura za wazi, walionekana kuwazidi kwa wingi wale wanaotaka kura za siri.
Wajumbe wa CCM ambao ni wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muunganom– Esther Bulaya na Profesa Juma Kapuya walijitoa mhanga na kueleza bayana kuwa hawako tayari kuona demokrasia ikikandamizwa kwa kulazimishwa kupiga kura za wazi. Akishangiliwa kwa nguvu, Bulaya alisisitiza kuwa hayuko tayari kulazimishwa kupiga kura ya wazi huku akijua kuwa utaratibu huo unamnyima uhuru wake.
“Nitasema kweli daima, fitina kwangu mwiko. Ni lini na wapi maamuzi magumu kama haya yalifanyika?” Alihoji mbunge huyo wa Viti Maalumu.
Bulaya alisema hakuna sheria inayomtaka mtu kushurutishwa kufanya uamuzi na kwamba kumtaka atoe sauti ya juu katika kura za wazi, ni kumlazimisha kufanya kinyume na matakwa yake.
Alisema kamwe hawezi kuuza uzalendo wake kwa kupiga kura za wazi na kwamba atapimwa kwa utashi wake kuhusu kile anachokiamini. Kwa upande wake, Profesa Kapuya alisema namna nzuri ya kumpa uhuru mpiga kura, ni kutomshurutisha ili afuate matakwa ya wengine.
Alisema kura za siri ndizo zitakazowaimarisha wajumbe na kwamba kinyume chake, kura za wazi zitawagawa na hatimaye kutoka bungeni wakiwa vipande vipande.
Kwa upande wake, Anna Kilango Malecela aliunga mkono ‘kiaina’ kura ya siri akisema alimsikiliza Profesa Ibrahim Lipumba kwa karibu saa nzima kupitia Kituo cha Televisheni ya Taifa (TBC), akamshawishi kutokana na hoja alizozitoa.
Alisema kwa kuwa suala hilo limezua mvutano mkubwa katika bunge hilo, ni bora likaamuliwa kwa kupigiwa kura ya siri.
Wajumbe wengine
Mjumbe wa Bunge hilo, Sheikh Mussa Kundecha aliunga mkono utaratibu wa kura ya siri akisema ndiyo pekee unaoweza kuwaunganisha wajumbe.