come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

TFF YASOGEZA MBELE MUDA WA USAJILI

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeongeza muda wa siku kumi wa kumalizika kwa usajili wa wachezaji wa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kutokana na kuchelewa kwa 'link' ya mfumo mpya wa usajili kutoka Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Kutokana na hilo, dirisha la usajili litafungwa Agosti 27, badala ya (jana) Agosti 17.Kwa mujibu wa CAF, link hiyo itakuwa tayari kwa matumizi ndani ya siku tatu zijazo kutoka sasa.

Ofisa Habari na Mawasiliano wa TFF, Boniface Wambura alisema mameneja wa usajili wa timu hizo kwa sasa wanatakiwa kukamilisha nyaraka zote zinazotakiwa ili 'link' hiyo itakapokuwa tayari waweze kuingiza usajili wao mara moja.


"Kuanzia msimu wa 2014/2015 mfumo unaotumika kwa usajili kwa klabu hizo ni wa elektroniki badala ya ule wa zamani wa kutumia fomu za kawaida," alisema Wambura.

Alisema mfumo huo wa kisasa ambao pia unatumiwa na CAF unaondoa upungufu uliokuwapo katika mfumo wa zamani.

Kutokana na mabadiliko hayo, dirisha la usajili sasa litamalizika Agosti 27 mwaka huu badala ya jana Agosti 17, huku kipindi cha timu kuweka pingamizi ni kuanzia Agosti 28 hadi Septemba 3 mwaka huu.

Alisema Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji itakutana kati ya Septemba 6 na 8 mwaka huu kwa ajili ya kupitia pingamizi na kuthibitisha usajili.

Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inayoshirikisha timu 14 itaanza Septemba 20 mwaka huu wakati ratiba inatarajia kutoka mwezi mmoja kabla ya kuanza ligi hiyo.

Ligi Daraja la Kwanza inatarajia kuanza wiki ya kwanza ya Oktoba.

Mwisho wa kuombewa Hati ya Uhamisho ya Kimataifa (ITC) kwa wachezaji wanatoka nje ya Tanzania ni Septemba 6 mwaka huu.