Mvutano mkali wa kisheria uliibuka jana Mahakama Kuu baada ya upande wa mashtaka kutaka kuongeza shahidi wakati wa usikilizwaji wa kesi ya dawa za kulevya inayomkabili raia wa Kenya, Mwanaidi Ramadhani Mfundo, maarufu kwa jina la Mama Leila na wenzake saba.
Ubishi mkali ulianza pale Wakili Mwandamizi wa Serikali, Prosper Mwangamila alipowasilisha ombi la kuongeza shahidi kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Eva Mamuya ambaye alizifanyia dawa hizo uchunguzi wa kimaabara.
Mbele ya Jaji Grace Mwakipesile anayesikiliza kesi hiyo, Mwangamila alisema: “Kwa vile kesi hii inahusu dawa za kulevya, tunaomba shahidi huyu aweze kupata nafasi ya kutoa ushahidi wake”.
Mwangamila ambaye anasaidiwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Peter Maugo aliongeza kuwa mashahidi wote watakaofika mahakamani watatoa ushahidi unaohusu dawa alizofunga Mamuya, hivyo lazima awepo mahakamni kwa ajili ya kuzifungua.
Kwa kuzingatia mazingira hayo, wakili huyo aliiomba Mahakama hiyo iahirishe kesi hiyo hadi leo, ili waweze kuwasilisha taarifa ya kumwongeza shahidi huyo katika mashahidi wao, kwa mujibu wa kifungu cha 289 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).
Hoja hiyo ilisababisha mabishano ya kisheria pale mawakili wa utetezi wakiongozwa na Yassin Membar walipopinga ombi kwa maelezo kwamba kifungu hicho kinautaka upande wa mashtaka kutoa sababu za kuridhisha za kutaka kumwongeza shahidi mpya, baada ya usikilizwaji wa awali wa kesi katika Mahakama za chini.
Usikilizwaji wa awali wa kesi hiyo ulifanywa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam. Mawakili hao pia waliutaka upande wa mashtaka kuendelea na ushahidi wa shahidi mwingine waliyekuwa wamemwandaa.
Wakili mwingine wa utetezi, John Mapinduzi aliomba Mahakama itupilie mbali ombi la Jamhuri, akidai kuwa linalenga kuwahujumu wateja wao na kwamba ushahidi huo haukuwapo awali, badala yake unataka kupikwa.
Jaji Mwakipesile baada ya kusikiliza hoja za pande zote aliahirisha shauri hilo hadi leo kwa ajili ya kutoa uamuzi wa ombi hilo la upande wa Jamhuri.
Mama Leila ambaye pia hujulikana kwa majina ya Naima Mohammed Nyakiniwa, anadaiwa kuwa mfanyabiashara wa dawa za kulevya wa kimataifa ambaye amewahi pia kutajwa na Rais wa Marekani, Barrack Obama, kuwa ni mtu hatari kwa biashara hiyo.
Katika kesi hiyo yeye na wenzake wanakabiliwa na shtaka la kuingiza nchini Tanzania dawa za kulevya aina ya Cocaine, zenye uzito wa kilo 5 ambazo zinadaiwa kuwa na thamani ya Sh225 milioni.
Washtakiwa wengine Antony Arthur Karanja na Ben Ngare Macharia (wote Wakenya); na Watanzania watano; Sarah Munuo, Almas Said, Yahya Ibrahim, Aisha Kungwi, Rajabu Juma Mzome na John William.