Wakati kocha Yanga, Ernest Brandts akitegemea kumuanzisha kiungo wake nyota Haruna Niyonzima 'Fabregas' kwenye mechi yao ya leo ya Ligi Kuu ya Bara dhidi ya Prisons, kocha wa wapinzani wao hao, Jumanne Chale amepania kuondoka na pointi tatu kwenye mechi hiyo ya kwanza kwenye uwanja wa nyumbani.
Brandts aliuambia mtandao huu jijini hapa jana kuwa kukosekana kwa nyota wake huyo raia wa Rwanda kulichangia kutoka sare ya 1-1 na Mbeya City kwenye mchezo wao wa Jumamosi na anamini nyota huyo atakuwa na msaada mkubwa katika kikosi chake katika mechi ya leo.
“Kikubwa kwangu ni kurejea uwanjani kwa Haruna. Hakuwapo kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya Mbeya City.. lakini kesho (leo) atakuwapo. Lengo letu ni kushinda ili tuondoke na pointi nne huku japo najua kuna ugumu wake kwa sababu wapinzani wetu (Prisons) pia wamejiandaa vizuri,” alisema Brandts.
Alisema kuwa pamoja na kurejea kwa Niyonzima, kikosi chake kitakachoanza leo hakitakuwa na tofauti kubwa na kilichocheza katika mechi yoao dhidi ya Mbeya City.
Kocha wa Prisons, Jumanne Chale aliwaambia waandishi wa habari jijini hapa jana kuwa timu yake imejipanga vizuri kuwakabili Yanga na imepania kufanya vizuri kwenye mchezo huo wa kwanza wakicheza kwenye uwanja wake wa nyumbani.
“Tunaiheshimu Yanga kwa sababu ni timu kubwa na ina wachezaji na makocha wazuri, lakini wachezaji wa Afrika hasa Afrika Mashariki na kati uwezo wao haupishani sana, tutawakabili vilivyo,” alisema Chale.
Alisema timu yake inahitaji kushinda mechi hiyo kwa kuwa haijashinda mchezo wowote tangu kuanza kwa ligi hiyo msimu huu ikiambulia pointi moja tu katika mechi tatu walizotoka suluhu dhidi ya Coastal Union na kupoteza michezo miwili dhidi ya Ruvu Shooting na vinara wa msimamo JKT Ruvu.
Tambo nyingine za kufanbya vizuri katika mechi za leo zimetolewa na makocha wa Simba na Mgambo JKT ambao timu zao zinakutana kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo jioni katika mechi nyingine ya raundio ya nne ya ligi hiyo itayokuwa chini ya Kamishna David Lugenge kutoka Iringa.
Kocha wa Simba, Abdallah Kibaden 'King' amesema timu yake haijabweteka na ushindi wa magoli 2-0 walioupata dhidi ya Mtibwa Sugar Jumamosi na leo watashuka dimbani kupambana ili kupata pointi nyingine tatu dhidi ya wageni Mgambo JKT.
"Mgambo ni timu ngumu, kwetu kila mechi ni muhimu na ninawaambia vijana waingie kwa lengo la kusaka ushindi, ubingwa unatokana na kupata matokeo mazuri katika mechi nyingi na si kuangalia ukubwa au jina la klabu unayopambana nayo," alisema kocha huyo katika mahoajiano maalum na gazeti hili jana.
Mohamed Kampira, kocha wa Mgambo JKT alisema jana kuwa kikosi chake kiko vizuri na wamejiandaa kulipiza kisasi cha kufungwa na Simba katika mechi yao ya mzunguko wa pili wa ligi hiyo msimu uliopita.
Vinara wa ligi hiyo, JKT Ruvu wanaonalewa na kocha Mbwana Makata watakuwa ugenini Uwanja wa Mabatini ulioko Mlandizi mkoani Pwani dhidi ya 'ndugu zao' Ruvu Shooting ya kocha Charles Boniface Mkwasa.
Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Oljoro JKT kutoka Arusha na wenyeji Kagera Sugar wakati Azam na Ashanti United zitakwaruzana kwenye uga wa Azam Complex ulioko Chamazi jijini Dar es Salaam.
Mwamuzi Jacob Adongo kutoka Mara ndiye atakayechezesha mechi kati ya Coastal Union na Rhino Rangers itakayofanyika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga. Mtibwa Sugar inarejea uwanja wake wa Manungu ulioko Turiani mkoani Morogoro kuwakaribisha Mbeya City ya kocha Juma Mwambusi.
Imeandikwa na Faustine Feliciane, Mbeya, Sanula Athanas na Somoe Ng'itu, Dar es Salaam.