Washindi wa zamani wa taji la taifa la urembo nchini, akiwemo malkia wa Afrika 2005, Nancy Sumary, wameteuliwa kuwa majaji wa shindano la mwaka huu linalotarajiwa kufanyika Jumamosi wiki hii kwenye Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.
Akizungumza jana, Mkurugenzi wa Kampuni ya Lino Agency International inayoandaa shindano hilo, Hashim Lundenga, aliwataja warembo wengine wa zamani walioteuliwa kuwa majaji kuwa ni pamoja na Miss Tanzania mwaka 2000, Jacquiline Ntuyabaliwe 'K-lyn', Faraja Kotta (2004), Genevieve Mpangala na Sophia Byanaku ambaye aliwahi kushiriki fainali hizo miaka iliyopita.
Lundenga alisema zoezi la kuwasaili warembo lilianza juzi na jana ambapo kabla ya kuanza mchakato huo, majaji wote walipewa semina maalumu ya kufahamu sifa za kumpata mshindi anayetakiwa.
"Pia wapo majaji wengine watatu ambao ni wanaume wanaotoka katika makampuni yaliyodhamini shindano letu," alisema Lundenga.
Aliongeza kuwa, warembo wote wanaendelea vema na maandalizi ya shindano hilo.
"Maandalizi yako katika hatua za mwisho, tunaahidi shindano hili litazidi kuwa bora kuliko linavyofanyika katika nchi nyingine barani Afrika," alisema Lundenga.
Kadhalika alisema wasanii wanaotarajiwa kusindikiza shindano hilo watajulikana leo baada ya jana jioni kukamilisha mazungumzo nao na kwamba watakuwa ni wa ndani na nje ya nchi.
Aliwataja warembo wanaotarajiwa kupanda jukwaani kuwania taji la Redd's Miss Tanzania linaloshikiliwa na Brigitte Alfred, kuwa ni Happiness Watimanywa, Sabrina Juma, Nice Jack Herman, Anastazia Donald, (Kanda ya Kati), Lina Allan, Jacquiline Luvanda, Neema Mality (Nyanda za Juu Kusini) huku kutoka Mashariki wakiwa ni Diana Laizer, Sabra Islam, Janet Awetu na Elizabeth Pert, wakati ambapo Lucy Charles, Eshy Rashid na Salsha Esdory wakitokea Kanda ya Ziwa.
Wengine ni Severina Lwinga (Ustawi wa Jamii), Miriam Manyanga (Chuo Kikuu Huria), huku kutoka Temeke wakiwa ni Lucy James, Svetlana Nyamweyo, Latifa Mohamed na Narietha Boniface.
Kutoka Kaskazini ni Nancy Moshi, Glory Minja na Mary Chemponda, wakati ambapo Lucy Tomeka, Prisca Clement, Philios George na Sarah Martin wakiiwakilisha Kinondoni, kadhalika Dorice Mollel, Alice Isaac na Caro Bayo watakuwa wakibeba dhamana ya Ilala.