come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

YANGA KUANZA NA GOR MAHIA KAGAME CUP

Mabingwa wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara, Yanga, wataanza kampeni ya kuwania ubingwa wa michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) kwa kuwakaribisha Gor Mahia ya Kenya katika mechi ya ufunguzi wa Kundi A itakayofanyika Julai 18, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Akitangaza ratiba hiyo jana jijini, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka la Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), Nicholas Musonye, alisema kuwa mechi hiyo itatanguliwa na michezo mingine miwili itakayowakutanisha APR ya Rwanda dhidi ya Al Ahly Shandy ya Sudan na KMKM ya Zanzibar dhidi ya Telecom ya Djibout.


Musonye alisema kuwa mashindano ya mwaka huu yatashirikisha timu 13 ambazo zimegawanywa katika makundi matatu. Timu nane zitakazofanya vizuri zitasonga mbele kucheza hatua ya robo-fainali.

Alisema kuwa mechi ya fainali ya mashindano hayo itapigwa Agosti 2 na timu zote zitatakiwa kuleta wachezaji wake wa kikosi cha kwanza na si vijana kama ambavyo Azam kutoka Tanzania Bara 'imetangaza'.

Alizitaja timu zinazotarajiwa kuwania ubingwa huo ulioachwa wazi na El Merreikh ya Sudan kuwa ni pamoja na Yanga, Gor Mahia, Khartoum National (Sudan), Telecom (Djibout) na KMKM ambazo ziko Kundi A wakati Kundi B linaundwa na APR, Al Shandy (Sudan), Lydia Lecademy B (Burundi), Heegan ya Somalia huku Kundi C likijumuisha Azam, Malakia (Sudan Kusini), KCC (Uganda) na Adama City ya Ethiopia.

"Azam bado hawajaandikiwa barua, ila wataandikiwa na watatakiwa kuthibitisha ushiriki wao kwa kuleta timu A katika mashindano haya, na tutawapa muda maalumu kwa ajili ya kuthibitisha ushiriki wao, wakienda tofauti na kanuni,
taratibu zitafuatwa," alisema Musonye.

Aliongeza kwamba michuano ya mwaka huu itarushwa hewani moja kwa moja na kituo cha televisheni cha Supersport na kuongeza kuwa wenyeji Tanzania Bara wamethibitisha kugharamia malazi na usafiri wa ndani kwa timu zote zitakazokuja kushiriki michuano hiyo.

Kabla ya ratiba hiyo haijatangazwa, Rais wa Cecafa, Leodegar Tenga, alianza kwa kuwashukuru viongozi wa Shirikisho la Soka Nchini (TFF) kwa kukubali kuwa wenyeji wa michuano hiyo ambayo ina lengo la kutoa nafasi kwa wachezaji wa ukanda huu kujitangaza.

Tenga alisema Kombe la Kagame ni mashindano ya kujivunia na wanamshukuru Mlezi wa Cecafa, Rais wa Rwanda, Paul Kagame, kwa kuendelea kuwapatia fedha za zawadi ambazo ni Dola za Marekani 60,000.

Rais huyo wa zamani wa TFF alisema pia kutokana na kukosekana kwa wadhamini zaidi, timu zote shiriki zitatakiwa kujilipia gharama ya usafiri wa kuja Dar es Salaam na hii si mara ya kwanza kwa klabu kujigharamia.

El Merreikh ilitangaza kujitoa kutetea ubingwa wake mapema tangu mwezi uliopita kutokana na kuwekeza nguvu kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambako imeingia hatua ya makundi.