come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

DEUS KASEKE AINOGESHA YANGA UWANJA WA TAIFA.

Na Elias John.

MCHEZAJI wa timu ya Yanga Deus Kaseke leo ameinogesha timu yake ya Yanga, baada ya kuichabanga timu ya Mgambo JKT ya Tanga mabao 2-1.

Mgambo ilikuwa ndiyo ya kwanza kujipatia goli la kuongoza kupitia kwa mchezaji wake Nassoro Gumbo kunako dakika ya nne tu ya mchezo.

Yanga inayosifika kwa kuvitendea haki viporo vyake, imejitutumua ipasavyo, ambapo kunako dakika za kukaribia kumalizika kwa kipindi cha kwanza walichomoa goli hilo kupitia kwa mchezaji wake Deus Kaseke.

Mpaka kufikia mapumziko timu zote zimetoka uwanjani kwa kutoshana nguvu ya goli moja kwa moja. Kipindi cha pili kimeanza kwa kasi ya timu zote kuwa na kiu ya kupata goli la kuongoza.

Katika kipindi hicho cha pili, Yanga walifanya mabadiliko kwa kumuingiza Donald Ngoma na Thaban Kamusoko. Mabadiliko hayo yaliongeza uhai katika timu ya Yanga ambayo kunako dakika ya 29 kipindi cha pili, ni Kaseke tena kaiandikia timu yake goli la pili baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa Haruna Niyonzima.

Ushindi huo umeipandisha Yanga hadi kileleni kwa kuwa na pointi 62 ikiwa imecheza michezo 25, nyuma ya Azam inayoshikilia nafasi ya pill kwa kuwa na pointi 58, ikifuatiwa na Simba inayoshikilia nafasi ya Tatu kwa kuwa na pointi 57.

Hadi mwisho wa mchezo huo wa leo Kati ya Yanga na Mgambo, matokeo yamebaki kuwa magoli mawili kwa Yanga na goli moja kwa Mgambo.