Na Elias John.
SIKU CHACHE baada ya Baraza la michezo la Taifa (BMT) kuliamuru Shirikisho la mpira wa miguu hapa nchini Tanzania (TFF) kusimamia uchaguzi wa klabu ya Yanga SC, tayari Shirikisho hilo limetangaza tarehe ya uchaguzi huo
Akizungumza na waandishi wa habari jana mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi ya Tff, Wakili Aloyce Komba amesema uchaguzi wa Yanga sasa utafanyika june 5 mwaka 2016.
Komba ametiririka kuwa mchakato wa uchaguzi huo utakuwa ni wa siku 33 na kwamba mbio zake zitaanza rasmi mei 3 mwaka 2016.
Ameongeza kuwa jukumu kubwa la wao katika uchaguzi huo ni kuhakikisha kwamba uchaguzi unakuwa wa uhuru na haki ili kuepusha manung'uniko yasiyo na tija kwa wagombea.
Katika hali isiyo ya kawaida Komba ameshindwa kuitaja moja kwa moja katiba itakayotumika katika uchaguzi huo na kudai kwamba Tff inaendelea kufanya udadavuaji na itakapojiridhisha kwamba ni katiba ipi itakayofaa kutumika katika uchaguzi huo itaweka bayana.
BMT imelitaka Shirikisho la mpira wa miguu hapa nchini Tanzania kusimamia uchaguzi wa klabu Yanga haraka kwa madai kwamba viongozi wa klabu hiyo kongwe hapa nchini yenye maskani yake mitaa ya Twiga na Jangwani wapo kinyume na utaratibu baada ya muda wao wa kuongoza klabu hiyo kisheria kumalizika.