Na Elias John.
MABINGWA watetezi wa ligi kuu Tanzania Bara na washiriki wa kombe la FA Yanga SC wameibuka na ushindi wa magoli 2-1 baada ya kuitandika Coastal Union ya mjini Tanga.
Coastal yenyewe ndio iliyotangulia kupata goli kupitia kwa mchezaji wake Youssef Sabo kunako dakika za mwanzo za kipindi cha pili.
Yanga nayo imekataa dharau ambapo kunako dakika za mwishoni katika kipindi cha pili waliweza kusawazisha goli hilo kupitia kwa mchezaji wake Donald Ngoma.
Mpaka dakika 90 za mchezo huo zinamalizika timu zote zimetoka uwanjani zikitoshana nguvu kwa kufungana goli 1-1.
Kutokana na matokeo hayo mwamuzi wa mchezo huo alilazimika kuongeza dakika 30 ili mshindi apatikane ndipo mshambuliaji wa Yanga raia wa Burundi Amis Tambwe akaiandikia timu goli la pili na la kuongoza.
Mchezo kati ya Coastal Union ya Tanga na Yanga SC ya jijini Dar es Salaam ilitawaliwa na fujo nyingi ambapo mashabiki wa timu ya soka ya Coastal Union walivurumisha uwanjani mawe pamoja na chupa za maji.
Nalo Shirikisho la mpira wa miguu hapa nchini Tff limesema wao wanasubiri ripoti ya kamisaa wa mchezo huo ili kuona ni hatua zipi za kuchukukua kutokana na vurugu zilizojitokeza katika mchezo huo.